-Bilioni 3.2 kutumika kukamilisha miradi Ludewa, Njombe
-Wananchi, taasisi za kijamii kuanza kunufaika na nishati ya REA
-Sekta za uvuvi, afya na elimu kupata mapinduzi makubwa
Ludewa, Njombe📍
Matumaini ya ukuaji wa uchumi na uboreshaji wa huduma za kijamii yameongezeka kwa wakazi wa mwambao wa Ziwa Nyasa, wilayani Ludewa, kufuatia hatua ya Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kufikisha miradi ya umeme kwenye vitongoji vya eneo hilo.
Katika ziara ya Bodi ya Nishati Vijijini (REB) iliyolenga kukagua maendeleo ya miradi hiyo mkoani Njombe, imebainika kuwa kiasi cha Shilingi Bilioni 3.2 kimetengwa kwa ajili ya kukamilisha miradi ya kusambaza nishati hiyo katika wilaya ya Ludewa.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo katika Shule ya Msingi Lumbila, Mwalimu Mkuu Msaidizi, John Mwasoso, amesema ujio wa umeme ni ukombozi katika mazingira ya kufundishia na kujifunzia. Alibainisha kuwa tayari wameanza maandalizi ya awali kwa kufanya mifumo ya nyaya (wiring) kwenye baadhi ya vyumba vya madarasa na nyumba za walimu.
Kwa upande wao, wananchi wa kitongoji cha mabatini wameonyesha shauku ya kutumia nishati hiyo kuchochea uchumi wao, hususan katika sekta ya uvuvi. Bwana Augustino Madesu, mkazi wa eneo hilo, alisema umeme utawasaidia kuhifadhi samaki kwa kutumia majokofu (friza), jambo litakalowaepushia hasara ya kuuza samaki kwa bei ya kutupa pindi wanapovua kwa wingi.
Naye Mganga Mfawidhi wa zahanati ya Nkanda, Timotheo Nkwabi, alieleza kuwa umeme utamaliza changamoto ya kutoa huduma za afya gizani wakati wa usiku na kuimarisha mifumo ya kidigitali ya utunzaji wa kumbukumbu za wagonjwa na dawa.
Mkurugenzi wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhandisi, Ahmed Chinemba, amewahakikishia wananchi kuwa serikali imeweka kipaumbele kwenye taasisi za umma kama shule, zahanati na miradi ya maji ili kuhakikisha wananchi wananufaika kwa haraka.
“Tunawahamasisha wananchi kujiandaa kwa kufanya ‘wiring’ kwenye majengo yao ili waweze kuupokea umeme mara tu unapofika. Lengo ni kuona nishati hii inabadilisha maisha ya mtanzania wa vijijini,” alisema Mhandisi, Chinemba.
Naye Kaimu Meneja Msimamizi wa Miradi REA, Mhandisi Deogratius Nagu, aliongeza kuwa kutokana na ongezeko la mahitaji, Bodi ya Nishati Vijijini (REB) imeelekeza kuongezwa kwa idadi ya wanufaika ili kuhakikisha kaya nyingi zaidi zinapata nishati hiyo kabla ya mradi kukamilika rasmi.
Kukamilika kwa mradi huu kunatarajiwa kufungua fursa mpya za ajira kwa vijana kupitia vijiwanda vidogo, saluni, na biashara nyinginezo zinazotegemea nishati ya umeme, huku kukiimarisha usalama na ustawi wa jamii katika mwambao wa Ziwa Nyasa.


.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...