Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma 

Serikali kupitia Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imetangaza mpango wake wa mwaka wa fedha 2026/2027 unaolenga kuimarisha ufanisi, uwazi na utoaji wa huduma bora katika utumishi wa umma.

Akiwasilisha hotuba ya bajeti bungeni Dodoma Aprili 17, 2026,Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete amesema serikali imeweka kipaumbele kikubwa katika ajira, ambapo jumla ya nafasi mpya 45,000 zinatarajiwa kujazwa ili kupunguza upungufu wa watumishi katika taasisi mbalimbali za umma.

Sambamba na hilo, vibali vya ajira mbadala 7,124 vitatolewa kuhakikisha utendaji kazi haukwami pindi watumishi wanapoondoka kazini kwa sababu mbalimbali.

Katika kulinda haki za watumishi, serikali imepanga kuhakiki na kuidhinisha madai ya malimbikizo ya mishahara katika taasisi 425, pamoja na kushughulikia madai ya wastaafu na waliokoma utumishi kutoka kwa waajiri 200. Pia, usimamizi wa malipo ya mishahara utaimarishwa katika taasisi 510 ili kuhakikisha malipo yanafanyika kwa wakati na kwa usahihi.

Kwa upande wa maboresho ya mifumo ya kiutumishi, serikali itafanya uhakiki wa watumishi (staff audit) katika taasisi 127 zinazotumia mfumo wa e-Watumishi, huku taasisi 35 ambazo bado hazijaanza kutumia mfumo huo zitawezeshwa kujiunga nao. Maboresho zaidi yatahusisha kuimarisha teknolojia ya mfumo huo na kuunganisha na mifumo mingine ya serikali pamoja na sekta binafsi.

Aidha, serikali imepanga kuanzisha mfumo maalum wa “dashboard” utakaokusanya na kuwasilisha takwimu sahihi kutoka mifumo mbalimbali ikiwemo e-Watumishi, e-Msawazo, e-Utendaji na Watumishi Portal, hatua inayotarajiwa kuboresha maamuzi ya kiutendaji katika ngazi zote za serikali.

Mpango huo unaonesha dhamira ya serikali ya kuendelea kuboresha utumishi wa umma kwa kuweka mifumo madhubuti, kuongeza ajira na kuhakikisha watumishi wanapata stahiki zao kwa wakati.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...