MSTAHIKI Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Alimwoni Chaula ameeleza kuwa jiji linaendelea kuthamini mchango wa wadau wa maendeleo katika kuimarisha mifumo ya chakula mijini kupitia ushirikiano unaolenga ustawi wa wananchi na maendeleo endelevu.

Akizungumza katika kikao cha wadau kuhusu uanzishwaji wa Jukwaa la Wadau wa Mifumo ya Chakula wa Jiji la Dodoma alianza kwa kuwashukuru watekelezaji wa Mradi wa Tukue kwa Pamoja “Growing Together” unaotekelezwa na IDH kupitia RIKOLTO kwa kuendelea kuwa mshirika muhimu wa Jiji la Dodoma katika safari ya kuimarisha mifumo ya chakula mijini.

“Kwa kutumia nafasi hii, napenda kuwashukuru kwa dhati watekelezaji wa Mradi wa Tukue kwa Pamoja kwa kuendelea kuwa mshirika wa karibu wa Jiji la Dodoma katika safari ya pamoja ya kuimarisha mifumo ya chakula mijini. 

Ushirikiano huu unaweka msingi imara wa kuhakikisha upatikanaji wa chakula salama, chenye lishe na kwa gharama nafuu tukizingatia jiji letu linakuwa kwa kasi. Kwahiyo, mahitaji ya mifumo madhubuti ya chakula lazima iwepo” alisema Chaula.

Aidha, alisema kuwa kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya tabianchi, kupanda kwa bei za bidhaa na utegemezi mkubwa wa chakula kutoka nje ya jiji, ipo haja ya kuwa na jukwaa la pamoja litakalowakutanisha wadau mbalimbali kwa ajili ya kupanga na kuratibu mikakati ya kuimarisha usalama wa chakula.

 “Uanzishwaji wa Jukwaa la Wadau wa Mifumo ya Chakula wa Jiji la Dodoma si hiari bali ni hitaji la msingi katika kuhakikisha tunakuwa na mfumo wa chakula ulio imara, jumuishi na endelevu” alisema Chaula.

Katika hatua nyingine, alisisitiza kuwa Jiji la Dodoma linaunga mkono kikamilifu uanzishwaji wa jukwaa hilo na lipo tayari kuhakikisha linaunganishwa katika mipango na mifumo rasmi ya halmashauri ili kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa sera zinazohusiana na lishe, afya, biashara na maendeleo ya miji.

Nae, Afisa Lishe Jiji la Dodoma, Semeni Eva Juma alisema kuwa chakula bora kinapaswa kuwa na virutubisho kamili. “Suala la kuwa na mifumo imara ya chakula tunapaswa kulipa kipaumbele kwasababu chakula bora na chenye afya inabidi kiwe katika makundi sita. Tunapongeza mradi huu, unatija kubwa sana katika kuboresha mifumo ya chakula. Tutaendelea kutoa elimu kwa jamii ili kujenga kizazi imara” alisema Juma.

Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeonesha kuwa kupitia ushirikiano madhubuti wa wadau mbalimbali, jukwaa hilo litakuwa chachu ya kuimarisha usalama wa chakula, kuongeza ustawi wa wananchi na kujenga mfumo wa chakula wenye uwezo wa kukabiliana na changamoto za sasa na zijazo.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...