KAMPUNI ya utoaji wa huduma za bima ya afya kwa waajiri, Vitality Health International (Africa), imebadilisha rasmi jina na sasa itafahamika kama Discovery Health – Global Health Solutions, hatua inayolenga kuimarisha utoaji wa huduma za afya kwa waajiri na wafanyakazi wao nchini Tanzania na katika bara la Afrika kwa ujumla.
Mabadiliko hayo yameanza rasmi Januari 1, 2026, huku kampuni hiyo ikieleza kuwa hatua hiyo inalenga kuendeleza huduma zake za afya kwa kuunganisha uzoefu wake wa muda mrefu na programu ya ustawi ya Vitality pamoja na teknolojia za kisasa za huduma za afya.
Akizungumza Johannesburg, Afrika Kusini, Mkurugenzi Mkuu wa Discovery Health – Global Health Solutions, Emma Knox, alisema licha ya kubadilika kwa jina la kampuni, dhamira yao ya kuhakikisha watu wanakuwa na afya bora na maisha yenye ustawi itaendelea kuwa ile ile.
“Ingawa jina letu linabadilika, ahadi yetu kwa wateja wetu na kusudi letu la msingi la kuwafanya watu wawe na afya njema na kulinda maisha yao vinaendelea kubaki vilevile,” alisema Knox.
Alieleza kuwa mabadiliko hayo yatawezesha kampuni hiyo kuimarisha ushirikiano wake na kampuni za bima za ndani barani Afrika pamoja na kuleta suluhisho mpya za afya zinazolenga mahitaji halisi ya waajiri na wafanyakazi wao.
Nchini Tanzania, kampuni hiyo itaendelea kushirikiana na Strategis Insurance, ushirikiano ulioanza mwaka 2024, kwa lengo la kutoa huduma bora za afya zinazokidhi mazingira ya ndani ya huduma za afya na mahitaji ya waajiri wa Kitanzania.
Kwa mujibu wa Knox, ushirikiano huo umeiwezesha kampuni kupanua huduma zake nchini huku ikiendelea kutoa suluhisho za afya zenye kuzingatia mahitaji ya soko la ndani.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Strategis Insurance, Dk. Malav Manek, alisema wana matumaini makubwa ya kuendelea kuimarisha ushirikiano huo kupitia Discovery Health – Global Health Solutions.
“Tunaendelea kujizatiti kutoa bidhaa za kibunifu zinazolenga kukidhi mahitaji ya wateja huku tukihakikisha kiwango cha juu cha huduma kwa wateja wetu,” alisema Dk. Manek.
Kupitia mfumo wake mpya wa Global Health Solutions, kampuni hiyo itaendelea kutoa huduma za usimamizi wa afya na “managed care” kwa kutumia uzoefu wa zaidi ya miaka 34 wa Discovery Health katika sekta ya afya nchini Afrika Kusini.
Discovery Health pia imeeleza kuwa itaendelea kuweka mkazo katika usimamizi bora wa huduma za matibabu, udhibiti wa hatari pamoja na matumizi ya mifumo ya kisasa ya taarifa za afya ili kuhakikisha wateja wanapata huduma bora kwa gharama endelevu.



.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...