Na Karama Kenyunko Michuzi Tv


MAHAKAMA Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imetoa siku saba kwa Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chadema Zanzibar, Said Mohamed na wenzake kuwasilisha kiapo kinzani kujibu maombi yaliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu.

Lissu amewasilisha kwa mara ya pili maombi ya kutaka kuunganishwa katika kesi ya mgawanyo usio sawa wa rasilimali baina ya Bara na Zanzibar baada ya maombi yake ya awali kukataliwa.

Uamuzi huo umetolewa leo Mei 25, 2026 na Jaji David Ngunyale wakati maombi hayo yalipotajwa kwa mara ya kwanza.

Jaji Ngunyale alitoa siku saba kwa Mohamed na wenzake kuwasilisha kiapo hicho, huku maombi hayo yakitarajiwa kusikilizwa Juni 2, 2026. Lissu alikuwepo mahakamani kufuatilia maombi yake.

Awali, Lissu alifungua shauri la maombi kwa jina lake binafsi, akiomba kuunganishwa katika kesi hiyo kama mdaiwa wa lazima, akidai kuwa ana masilahi makubwa katika kesi hiyo kwa kuwa ndiye mwenyekiti wa chama na kwamba uamuzi wowote utamuathiri.

Hata hivyo, Mahakama hiyo baada ya kusikiliza hoja za pande zote, katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Hamidu Mwanga aliyekuwa akiisikiliza kesi ya msingi pamoja na maombi hayo, ilimkatalia rasmi Lissu kujumuishwa katika kesi hiyo.

Katika uamuzi huo uliosomwa Alhamisi Aprili 30, 2026 na Naibu Msajili Hussein Mushi, Jaji Mwanga alisema Lissu hakuonesha alikuwa na masilahi ya karibu yanayomwezesha kustahili kuunganishwa katika kesi hiyo kwa jina lake binafsi.

Kutokana na uamuzi huo, Lissu amefungua maombi mapya akitumia cheo chake cha Mwenyekiti wa Chadema badala ya kutumia jina lake binafsi.

Shauri hilo limefunguliwa na Mohamed pamoja na wajumbe wawili wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema kutoka Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu dhidi ya Bodi ya Wadhamini waliosajiliwa wa Chadema na Katibu Mkuu wa chama hicho.

Walalamikaji wanadai kumekuwa na mgawanyo usio sawa wa mali za chama na rasilimali za kifedha kati ya Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara, kinyume na Sheria ya Vyama vya Siasa na Katiba ya chama hicho.

Wadai pia walifungua shauri dogo la maombi ya zuio la muda dhidi ya wadaiwa, wakitaka wasijihusishe na shughuli za kisiasa wala matumizi ya mali za chama hadi kesi ya msingi itakapoamuliwa.

Aidha, wanadai kuwepo kwa ubaguzi wa kidini na kijinsia pamoja na utoaji wa maoni na matamko yenye nia ya kuvuruga Muungano kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...