Na; Mwandishi Wetu Arusha
OFISI ya Makamu wa Rais inatarajiwa kuzindua Programu ya Kitaifa ya Mageuzi ya Kimkakati ya Mazingira Endelevu Tanzania katika kilele cha Siku ya Mazingira Duniani (WED) ambapo kitaifa itafanyika jijini Dodoma, Juni 5, 2026.
Akizungumza katika uzinduzi wa usafi wa Mazingira kuelekea siku hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni alisema lengo ni kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya mfano duniani katika suala la Uhifadhi na Utunzaji wa Mazingira.
Alisema Programu hiyo inalenga kutekeleza Dira, 2050 hususan nguzo ya tatu kuhusu Uhifadhi wa Mazingira na Ustahimilivu wa Mabadiliko ya Tabianchi ikiwa na lengo la kupanda miti bilioni 2 kwa mwaka, kuimarisha Biashara ya Kaboni, Uanzishaji wa Bustani za Kijani katika Miji na shughuli zingine za Kijani.
“Pia program hii inatarajia kuongeza ajira zinazoweza kufikia zaidi ya elfu ishirini na tano (25,000) ifikapo 2030 kupitia sekta za taka, misitu, kaboni na nishati safi,”alisema Mhe. Masauni.
Alifafanua kuwa tukio hilo ni sehemu ya juhudi za Kitaifa na Kimataifa za kulinda mazingira, kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kujenga jamii yenye afya na ustahimilivu.
Aidha, alileza Dira, 2050 imeweka maono ya Taifa kuwa hadi kufikia mwaka 2050 Tanzania iwe kinara katika matumizi endelevu ya rasilimali, Taifa linalotumia taka kama malighafi kwa manufaa ya kiuchumi na Taifa kinara katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kuimarisha ustahimilivu na uendelevu wa mazingira.
“Juhudi zinahitajika ili kutekeleza shughuli za mazingira kwa njia jumuishi inayohusisha makundi yote ya kijamii bila kujali jinsia au umri. Kwa jiji la Arusha, tafiti za mwaka 2020 zinaonesha kuwa jiji linazalisha takribani tani 550 za taka ngumu kwa siku, ambapo zaidi ya asilimia 60 ya taka hizo zinaweza kurejelezwa ikiwa zitadhibitiwa vizuri kupitia uchumi rejeshi,"aliongeza.
"Kwa ngazi ya Kitaifa, Tanzania inakadiriwa kupoteza takribani hekta 469,420 za misitu kila mwaka kutokana na shughuli mbalimbali zisizo endelevu ikiwa ni pamoja na matumizi makubwa ya kuni na mkaa, kilimo kisicho endelevu, ufugaji holela pamoja na shughuli nyingine za kibinadamu zinazosababisha uharibifu wa mazingira hali inayochangia kuongezeka kwa gesi joto, kuharibu vyanzo vya maji na kuhatarisha usalama wa bioanuwai,".
Alieleza Upandaji wa miti yenye matumizi mbalimbali una mchango mkubwa katika kufyonza gesi ya kaboni, kupunguza mmomonyoko wa udongo, kuhifadhi vyanzo vya maji, kutoa matunda pamoja na kuongeza kipato kwa wananchi kupitia bishara ya Kaboni na kuongeza ustahimilivu dhidi ya athari za Mabadiliko ya Tabianchi.
"Matumizi ya nishati safi ya kupikia ni hatua muhimu katika kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa ambao umeendelea kuwa miongoni mwa sababu kuu za uharibifu wa misitu nchini.
“Kuimarisha upatikanaji na matumizi ya nishati safi kama vile gesi asilia, umeme, biogas na teknolojia bora za kupikia kutasaidia kupunguza kasi ya ukataji miti, kupunguza uzalishaji wa gesi joto na kuboresha afya za wananchi hususan wanawake na watoto ambao huathirika zaidi na moshi unaotokana na matumizi ya nishati isiyosafi," alisisitiza.
Naye Mkuu wa Wilaya Arusha Mhe. Joseph Mkude alisema kila mmoja ana wajibu wa kutunza na kuhifadhi mazingira na kuzingatia matumizi ya nishati safi ya kupikia na kusema taasisi nyingi zinatekeleza agizo hilo.
Amesema arusha imekuwa ikifanya kila jitihada kuhakikisha jiji hilo linakuwa safi na kushirikisha jamii yote kutambua umuhimu wa utunzaji wa mazingira ndio maana wanafunzi wamepewa kipaumbele.
.jpg)



.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...