Na Mwandishi Wetu, Dodoma
SPIKA wa Bunge, Mussa Azan Zungu, ameibana Wizara ya Ujenzi akitaka mageuzi ya haraka katika utekelezaji wa miradi ya miundombinu kupitia mfumo wa Ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP), akionya kuwa kuendelea kutegemea serikali pekee kugharamia barabara ni mzigo mkubwa kwa taifa.
Katika msisitizo wake, Zungu alisema Tanzania haiwezi kufanikisha kikamilifu malengo ya maendeleo ya miundombinu bila kuipa nafasi sekta binafsi kushiriki katika uwekezaji wa barabara na miradi mingine mikubwa. Alieleza kuwa mataifa mengi duniani tayari yamepiga hatua kwa kutumia PPP kama suluhisho la changamoto za kifedha kwenye sekta ya miundombinu.
Amesema wakati umefika kwa Wizara ya Ujenzi kuacha kusita na kuonyesha dhamira ya kweli ya kuingia kwenye ubia huo, akibainisha kuwa mahitaji ya barabara nchini yanaendelea kuongezeka huku uwezo wa serikali kugharamia kila kitu ukiendelea kuwa finyu.
Zungu alikumbusha kuwa katika utekelezaji wa Vision 2050, sehemu kubwa ya miradi ya maendeleo inayokadiriwa kufikia asilimia 70 — inatarajiwa kutekelezwa kwa kushirikisha sekta binafsi, jambo linalofanya mfumo wa PPP kuwa sehemu muhimu ya mkakati wa taifa wa maendeleo.
Akionyesha kutoridhishwa kwake na kasi ya wizara hiyo, Spika huyo alihoji mantiki ya serikali kuendelea kubeba mzigo mkubwa wa utekelezaji wa miundombinu peke yake wakati fursa ya kugawana gharama na majukumu ipo wazi kupitia sekta binafsi.
Kauli ya Zungu imekuja kama shinikizo jipya kwa Wizara ya Ujenzi kuharakisha mageuzi ya namna miradi ya miundombinu inavyotekelezwa, huku akisisitiza kuwa ubia wa PPP sasa ni lazima waonekane kama suluhisho la maendeleo badala ya chaguo la hiari.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...