Na Mwandishi wetu.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kusisitiza dhamira yake ya kuhakikisha watu wenye ulemavu wanashiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa kupitia utekelezaji wa sera, sheria, mipango na mikakati mbalimbali inayolenga kuondoa vikwazo vinavyowakwamisha kupata haki na huduma muhimu.

Kauli hiyo imetolewa leo Mei 26, 2026 jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Dkt. James Kilabuko wakati akifungua kikao kazi cha utekelezaji wa sera, miongozo na ujumuishaji wa watu wenye ulemavu kilichowakutanisha wadau mbalimbali kutoka taasisi za Serikali, mashirika na sekta binafsi.

Dkt. Kilabuko amesema Serikali inaendelea kutambua mchango mkubwa wa watu wenye ulemavu katika maendeleo ya kijamii, kisiasa na kiuchumi, ndiyo maana imeendelea kuweka mazingira wezeshi yatakayohakikisha kundi hilo linapata haki, fursa sawa pamoja na huduma bora kama wananchi wengine.

Amesema hatua mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa ikiwemo utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2004 pamoja na Sheria ya Watu Wenye Ulemavu Na. 9 ya mwaka 2010 sambamba na kanuni na miongozo mbalimbali inayolenga kuondoa vikwazo vya ushiriki katika nyanja tofauti za maendeleo.

“Serikali inaendelea kuweka mazingira rafiki kupitia sera, sheria, mipango na mikakati ili kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata haki, huduma bora na fursa sawa kama wananchi wengine,” amesema Dkt. Kilabuko.

Ameongeza kuwa Tanzania pia imeridhia Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Watu Wenye Ulemavu (CRPD) pamoja na mikataba mingine ya kikanda na kimataifa inayosisitiza usawa, utu na ujumuishaji wa watu wenye ulemavu katika shughuli za maendeleo.

Kwa mujibu wa Dkt. Kilabuko, hatua hiyo inaonyesha wazi dhamira ya Serikali ya kuhakikisha hakuna mwananchi anayebaki nyuma katika safari ya maendeleo ya Taifa.

Hata hivyo, amesema pamoja na mafanikio yaliyopatikana bado zipo changamoto mbalimbali zinazokwamisha utekelezaji wa masuala ya ujumuishaji, ikiwemo uelewa mdogo wa jamii kuhusu haki za watu wenye ulemavu, upungufu wa huduma jumuishi katika baadhi ya sekta pamoja na changamoto za utekelezaji wa sera na sheria katika ngazi tofauti.

Amesema changamoto hizo zinahitaji ushirikiano mkubwa wa wadau wote ili kuhakikisha mazingira yanakuwa rafiki zaidi kwa watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Watu Wenye Ulemavu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Wambura Kizito amesema kikao hicho kimekusudia kuwakutanisha wadau wa huduma kwa watu wenye ulemavu ili kujadili kwa pamoja namna bora ya kuboresha utekelezaji wa huduma hizo kwa kuzingatia misingi ya ujumuishaji.

Amesema bado kuna changamoto za kimazingira na mawasiliano ambazo mara nyingi huwafanya watu wenye ulemavu kushindwa kushiriki ipasavyo katika huduma na mipango mbalimbali inayotolewa na Serikali pamoja na taasisi nyingine.

“Tumekutana hapa ili kwa pamoja tujadili namna ya kuondoa vikwazo vilivyopo na kuweka mazingira yatakayowawezesha watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika mipango ya maendeleo,” amesema Wambura.

Naye Meneja Programu wa Shirika la Sight Savers Tanzania, Edwin Maleko, akizungumza kwa niaba ya wadau wa mashirika mbalimbali, ameipongeza Serikali kwa hatua inazoendelea kuchukua katika kusimamia haki za watu wenye ulemavu na kuahidi kuendelea kushirikiana nayo kuhakikisha matokeo chanya yanapatikana katika jamii.

Maleko amesema ushirikiano kati ya Serikali, mashirika na wadau wengine ni muhimu katika kujenga jamii jumuishi inayotoa nafasi sawa kwa kila mwananchi bila ubaguzi.

Kikao hicho kimewakutanisha wadau mbalimbali wanaojihusisha na utoaji wa huduma kwa watu wenye ulemavu kutoka taasisi tofauti nchini kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa sera na mikakati ya ujumuishaji nchini.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...