MRADI wa ECOFISH unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Denmark kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Shirika la Denmark la Maendeleo ya Kimataifa (DANIDA), unaendelea kuboresha shughuli za uvuvi kwa jamii ya Pwani na kuimarisha huduma za tahadhari za mapema za hali ya hewa nchini.

Katika utekelezaji wa mradi huo, wataalamu kutoka TMA walikutana na wavuvi pamoja na wakulima wa Mwani kwa lengo la kujionea hali halisi ya shughuli zao za kiuchumi na changamoto zitokanazo na mabadiliko ya hali ya hewa wanazokabiliana nazo, sambamba na kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa katika shughuli za uvuvi na kilimo cha Mwani. Ziara hiyo iliambatana na semina maalum iliyowakutanisha wavuvi na wakulima wa Mwani ikiwa ni sehemu ya juhudi za mradi huo katika kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa matumizi ya taarifa za hali ya hewa katika kufanya maamuzi sahihi na salama.

Akizungumza katika semina hiyo, Mtaalamu wa Hali ya Hewa kutoka TMA na msimamizi wa mradi, Dkt. Sarah Emerald Osima, alisema mradi wa ECOFISH una mchango mkubwa katika kuimarisha huduma za hali ya hewa na ustahimilivu wa jamii za Pwani kupitia tafiti, elimu na teknolojia za tahadhari za mapema.

Dkt. Sarah aliendelea kusema mradi huo pia umewezesha udhamini wa masomo kwa wanafunzi saba wa shahada za uzamili na uzamivu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), Taasisi ya Sayansi za Bahari ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (IMS) pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ambapo mmoja wao ni mfanyakazi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA). Alisema hatua hiyo inalenga kujenga wataalamu watakaosaidia sekta ya uvuvi na hali ya hewa kwa siku zijazo.

Aidha, wananchi wa kisiwani hapoo wamepongeza mradi huu wa ECOFISH na TMA kwa kuwapatia elimu hiyo, wakisema imewasaidia kuelewa na kutumia taarifa za hali ya hewa katika kupanga shughuli zao za uvuvi.

“Sasa tunajua umuhimu wa kutafuta na kutumia taarifa za hali ya hewa, jambo ambalo hapo awali tulikuwa tunalifanya kwa uelewa mdogo. Kwa sasa tumejifunza mambo mengi ikiwemo namna ya kutafsiri taarifa hizo kama zinavyotolewa na wataalamu,” alisema Afisa Uvuvi kutoka Wilaya ya Wete, Ndugu,Suleiman Ali Amadi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...