
Na Karama Kenyunko Michuzi TV
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) kupitia chuo chake cha kodi imeanza mchakato wa kuandaa programu mpya ya Masters Degree in Taxation, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuandaa wahitimu wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira.
Akizungumza katika mkutano wa ushirikishwaji wa wadau uliofanyika chuoni hapo, Naibu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi Dkt Lewis Ishemoi alisema lengo la kuwakutanisha wadau mbalimbali ni kupata maoni yatakayosaidia kuandaa mtaala unaokidhi mahitaji ya soko.
Alisema wadau kutoka ndani ya TRA na sekta mbalimbali wamealikwa kutoa maoni kuhusu aina ya ujuzi unaohitajika kwa mhitimu wa kiwango hicho.
"Tumewaalika wadau mbalimbali ili kupata mawazo kuhusu ujuzi unaohitajika kwa mhitimu wa kiwango hicho kwa lengo la kutengeneza mitaala inayojibu matakwa ya soko," alisema.
Alieleza kuwa wamewashirikisha wataalamu wa kodi, sera na wadau kutoka nje ya mamlaka ili kutimiza matakwa ya taasisi zinazosimamia elimu ikiwemo NACTVET na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).
Kwa mujibu wake, programu hiyo ya Shahada ya Uzamili ya Kodi itakuwa ya vitendo zaidi ili kumwezesha mhitimu kuingia moja kwa moja kwenye soko la ajira akiwa na uwezo wa kukidhi mahitaji ya waajiri.
"Hii italenga kumtoa mtu ambaye anahitimu aende moja kwa moja kufanya kazi na aweze kukidhi matakwa ya mwajiri," alisema.
Kuhusu muda wa kuanza kwa programu hiyo, alisema hatua ya sasa ni ya kukusanya maoni ya wadau kabla ya kuendelea na hatua nyingine za maandalizi.
"Tunategemea mwaka huu, Mungu akijalia, tunaweza kuanzisha programu hii," alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Mafunzo ya Uzamili Praygod Chao alisema uamuzi wa kuanzisha Shahada hiyo umetokana na uhitaji mkubwa wa wataalamu wenye utaalamu maalumu katika masuala ya kodi.
Alisema kabla ya kuanza maandalizi ya programu hiyo, chuo kilifanya tathmini ya mahitaji ya soko la ajira (Training Needs Assessment) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
"Tulikwenda sokoni kuwauliza waajiri ni maeneo gani yanakosekana kwa wahitimu wetu. Hivyo tumebuni shahada hii ili kuziba pengo hilo na kuongeza utaalamu wa kodi pamoja na kuongeza compliance ya ulipaji wa kodi," alisema.
Aliongeza kuwa programu hiyo itanufaisha watumishi wa TRA, kampuni za ukaguzi wa hesabu, kampuni za kodi pamoja na mashirika mbalimbali yanayohitaji wataalamu wa kodi wenye ujuzi wa juu.
Naye Tax Partner kutoka Kampuni ya Ernest & Young (EY), Donald Nsanyiwa, alisema ushirikishwaji wa sekta binafsi katika maandalizi ya programu hiyo ni hatua muhimu itakayosaidia kuhakikisha mtaala unaandaliwa kwa kuzingatia mahitaji halisi ya waajiri.
"Tunapongezwa kuona wameamua kutushirikisha wadau wa nje. Hii itasaidia kuhakikisha programu itakayokamilika inakidhi mahitaji ya sekta binafsi," alisema.



.jpeg)

.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...