Na Mwandishi Wetu.

WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umezidi kujipambanua kama muhimili na nguzo madhubuti katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa, kupitia mikakati yake endelevu inayolenga kurasimisha shughuli za kiuchumi na kuhakikisha hakuna Mtanzania anayeachwa nyuma katika upatikanaji wa huduma za sajili na leseni.

Hayo yamebainishwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa, alipokuwa akifungua kikao kazi cha wafanyakazi wa Wakala hiyo kilichofanyika mkoani Morogoro ambapo ametumia nafasi hiyo kuelezea kwa kina mafanikio ya wakala huo katika kuendelea kuwahudumia Watanzania.

“Katika mwaka wa fedha wa 2025/2026, BRELA imefanikiwa kuvuka malengo na kutekeleza majukumu yake ya msingi kwa ufanisi mkubwa ikijikita katika kuboresha huduma kwa wadau, kuimarisha mifumo ya kidijitali, kupanua wigo wa urasimishaji biashara nchini licha ya changamoto za kimazingira na kiuchumi zilizojitokeza” amesema Nyaisa

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Sehemu ya Mipango, Utafiti na Ubunifu wa BRELA Alinda Lema, amebainisha mafanikio hayo yamepatikana kupitia usimamizi thabiti wa Mpango Mkakati wa miaka mitano wa 2021/22–2025/26.

Amefafanua katika kipindi cha kuanzia Julai 2025 hadi Juni 2026, mpango huo umewezesha mazingira ya biashara nchini kwa kuimarisha huduma za sajili na leseni, mifumo ya kiteknolojia, na usimamizi wa utendaji kazi wa watumishi.

Pia kumekuwa na ongezeko la kasi ya urasimishaji wa biashara, kuimarika kwa ulinzi wa haki miliki, na kurahisishwa kwa huduma zote zinazowafikia wadau wa sekta binafsi na ya umma.

“Kampuni zilizosajiliwa nchini zilipanda kutoka 18,541 katika mwaka wa fedha uliopita wa 2024/25 na kufikia kampuni 19,264 katika mwaka wa fedha wa 2025/26, ikiwa ni ongezeko la asilimia 4 linaloakisi kuongezeka kwa imani ya wawekezaji wa ndani na nje.

“Katika urasimishaji wa biashara, usajili wa majina ya biashara uliongezeka kutoka majina 31,123 hadi kufikia 35,362, ikiwa ni ongezeko la asilimia 14,”amesema Lema.

Kwa upande wa sekta ya viwanda na miliki ubunifu nayo haikuachwa nyuma, kwani ilionyesha ukuaji unaochochea azma ya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na uchumi wa kati.

Lema ameeleza kuwa utoaji wa leseni za viwanda uliongezeka kwa asilimia 50, kutoka leseni 435 hadi leseni 651 katika kipindi cha mwaka mmoja tu.

Pia utoaji wa Hataza kwa ajili ya kulinda wavumbuzi wa ndani ulishuhudia mapinduzi kwa kuongezeka kutoka hataza 30 hadi 61, ambalo ni ongezeko la asilimia 103, wakati usajili wa alama za biashara na huduma (Trade and Service marks) ukiongezeka kwa asilimia 10 kutoka sajili 3,148 hadi kufikia 3,455, hatua inayolinda alama na ubunifu wa wafanyabiashara sokoni.

BRELA ilitekeleza zoezi la kaguzi elimishi kwa upande wa leseni katika soko kuu la kimkakati la Kariakoo jijini Dar es Salaam. Ukaguzi huo haukulenga kuadhibu, bali kuweka mazingira rafiki ya uendeshaji biashara na uwekezaji kwa kutoa elimu ya uzingatiaji wa sheria za nchi.

Kuhusu uwazi na udhibiti wa mifumo ya kifedha, Wakala huo ulifanikiwa kufanya ukaguzi wa kina wa taarifa za wamiliki manufaa katika mkoa wa Arusha, hatua iliyosaidia kuongeza uelewa na kupunguza makosa yaliyokuwa yanajitokeza katika mfumo wa usajili wa kampuni.

Mkakati huu wa ukaguzi ulienda sambamba na utoaji endelevu wa elimu kwa umma kuanzia Julai 2025 hadi Juni 2026, ambapo BRELA ilitumia mbinu mbalimbali za kisasa kuwafikia wananchi.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...