MKURUGENZI wa Rasilimali Watu na Utawala wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),  Moshi Kabengwe, amewataka viongozi wa taasisi hiyo kuzingatia afya ya akili kwa watumishi wanaowasimamia kwa kuwa karibu nao na kujenga mazingira bora ya kazi yatakayowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Kabengwe ametoa rai hiyo jijini Dar es Salaam wakati wa kufungua mafunzo juu ya masuala ya afya ya akili na ushauri nasaha kwa viongozi wa TRA kwa mkoa wa Dar es Salaam 

Amesema mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za TRA za kuendelea kujenga mazingira bora ya kazi ili watumishi waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kuchangia kikamilifu katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

"Mapato ya kodi ndiyo yanayowezesha utoaji wa huduma mbalimbali za jamii, hivyo ni muhimu kila mmoja wetu awe na afya njema kimwili na kiakili ili aweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo," amesema Bw.Kabengwe.

Ameeleza kuwa kupitia mafunzo hayo, Kiongozi wanapatiwa maarifa ya kutambua dalili na viashiria vya msongo wa mawazo kwa watumishi, jambo litakalowasaidia kuchukua hatua za mapema kabla changamoto hizo hazijaathiri utendaji kazi.

Kabengwe amesema kiongozi anapaswa kuwa karibu na watumishi wake na kujenga mahusiano mazuri yatakayowafanya wajisikie huru, kuthaminiwa na kuwa na hamasa ya kufika kazini kila siku.

"Ukiona dalili kwamba mtumishi anaelekea kupata changamoto ya afya ya akili, ni muhimu kuanza kuchukua hatua za haraka za kumsaidia na kuweka mikakati ya muda mrefu ya kumwezesha kurejea katika hali yake ya kawaida," amesema.

Ameongeza kuwa viongozi wanapaswa kuwashauri watumishi wao na kuwaelekeza njia sahihi za kupata msaada wanapokabiliwa na changamoto mbalimbali za kisaikolojia.

Amesisitiza kuwa afya ya akili ni suala muhimu katika kuongeza tija mahali pa kazi na kwamba viongozi wana wajibu wa kuhakikisha wanatengeneza mazingira salama, yenye ushirikiano na yanayowajali watumishi wote.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...