Na Janeth Raphael MichuziTv - Bungeni Dodoma

Serikali ya Tanzania inaendelea kuchukua hatua kubwa za kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kupitia uanzishaji wa Mfumo wa Kidigitali wa One Stop Centre unaolenga kuunganisha taasisi mbalimbali za umma katika kutoa huduma kwa wawekezaji kwa njia rahisi na ya kisasa.

Akijibu swalibungeni leo, Naibu Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji) Dkt. Pius Chaya amesema mfumo huo unatekelezwa kwa awamu mbili, lengo likiwa ni kurahisisha upatikanaji wa huduma, kupunguza urasimu na kuongeza ufanisi katika sekta ya uwekezaji nchini.

Amefafanua kuwa awamu ya kwanza ya mfumo huo tayari imekamilika ambapo taasisi muhimu zimeunganishwa, zikiwemo Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na Idara ya Uhamiaji. Kupitia muunganiko huo, huduma kama usajili wa miradi ya uwekezaji, uhakiki wa kampuni, uhakiki wa vitambulisho vya taifa na uhakiki wa pasipoti sasa zinafanyika kwa mfumo mmoja wa kidigitali kwa ufanisi zaidi.

Aidha, serikali imeeleza kuwa awamu ya pili ya utekelezaji itapanua zaidi mfumo huo kwa kuunganisha huduma nyingine muhimu ikiwemo usajili wa kampuni, vibali vya makazi, namba ya utambulisho wa taifa (NIN), namba ya mlipakodi (TIN), msamaha wa kodi pamoja na vibali vya kazi. Hatua hiyo inalenga kuhakikisha wawekezaji wanapata huduma zote muhimu kupitia sehemu moja ya kidigitali.

Serikali imesisitiza kuwa lengo kuu la mfumo huo ni kuboresha mazingira ya biashara nchini kwa kupunguza muda wa mchakato wa kupata huduma, kupunguza gharama na kuongeza uwazi na ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Kwa ujumla, Mfumo wa One Stop Centre unatarajiwa kuwa chachu ya kuvutia uwekezaji zaidi nchini kupitia huduma jumuishi za kidigitali zinazowezesha urahisi wa kufanya biashara.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...