SAFARI ya miaka 30 ya mabadiliko katika sekta ya elimu nchini imeendelea kuandikwa na Dar es Salaam Independent School (DIS), shule iliyoanzishwa mwaka 1996 na Mama Susan L. Huxtable kwa lengo la kutoa elimu yenye viwango vya kimataifa kwa Watanzania, wakiwemo wale wenye uwezo wa kawaida wa kiuchumi.
Tangu kuanzishwa kwake, shule hiyo imekuwa ikitoa elimu kwa mtaala wa Cambridge huku ikijikita katika kuwajengea wanafunzi uwezo wa kufikiri, kufanya maamuzi na kujitegemea kupitia mchanganyiko wa masomo ya nadharia na vitendo.
Mkuu wa shule hiyo, Catherine Shindika, amesema mafanikio ya DIS yanaonekana kupitia wahitimu wake ambao wameendelea kufanya vizuri katika taasisi mbalimbali za elimu na maeneo ya kazi ndani na nje ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa maadhhimisho ya miaka 30 ya shule hiyo, yaliyofanyika Mbweni campus Dar es Salaam, Shindika, ambaye amejiunga na shule hiyo mwaka 1998 na kuhudumu kwa miaka 28, alisema shule hiyo imeendelea kujijengea sifa kutokana na ubora wa wanafunzi wake.
“Shule yetu inatangazwa na wahitimu wetu. Wanapohamia shule nyingine au kuingia katika ajira, uwezo wao huwavutia walimu na waajiri kiasi cha kuhoji walikotoka. Huo ndiyo ushahidi wa ubora wa elimu tunayotoa,” alisema.
Aliongeza kuwa DIS imekuwa mfano wa kuigwa hata kwa mamlaka za elimu, akibainisha kuwa wakati wa ukaguzi wa serikali, maofisa kutoka Wizara ya Elimu walivutiwa na mfumo wa ukaguzi wa ndani wa shule hiyo na kujifunza baadhi ya mbinu zinazotumika.
Kwa upande wa wazazi, Monicha Nyangasa ambaye ana watoto wawili wanaosoma katika shule hiyo, alisema DIS imekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya watoto wake kielimu na kijamii.
“Unaona mabadiliko ya watoto kila siku. Wamekua katika elimu, kujiamini na kujitambua. Kitu kizuri zaidi ni kwamba shule inashirikisha wazazi katika kila hatua, hivyo tunashuhudia maendeleo hayo moja kwa moja,” alisema.
Naye mzazi mwingine, Paul Bomani ambaye pamoja na kuwa na watoto wawili shuleni hapo yeye pia alihitimu kidato cha nne hapo hapo mwaka 1998 alisema shule hiyo imeweka mazingira yanayowakuza wanafunzi kuwa wabunifu na washiriki wa maamuzi yanayowahusu.
Alitolea mfano wa mchakato wa kuchagua sare za shule, ambapo wanafunzi walishiriki katika maonesho ya mitindo na kutoa maoni yaliyosaidia kupatikana kwa muonekano wa sare zinazotumika sasa.
“Hii inaonyesha namna wanafunzi wanavyopewa nafasi ya kufikiri, kubuni na kushiriki katika kufanya maamuzi. Ni sehemu ya kuwajenga kuwa viongozi wa baadaye,” alisema.

Kwa upande wa wanafunzi, Widad Hamis alisema mbali na masomo ya darasani, DIS imekuwa ikiwapa maarifa yanayowasaidia kuishi vizuri katika jamii na kukabiliana na mahitaji ya dunia ya sasa.
“Hapa tunajifunza namna ya kuishi na watu wengine, kujenga mahusiano mazuri na kutumia teknolojia katika maisha ya kila siku. Shule imewekeza sana katika kutufundisha teknolojia na kutuandaa kwa maisha ya baadaye,” alisema.
Kadiri DIS inavyoadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa kwake, shule hiyo inaendelea kuwa sehemu ya taasisi zilizochangia kukuza elimu ya kisasa nchini, huku ikijenga kizazi cha vijana wenye maarifa, ubunifu na uwezo wa kushindana katika mazingira ya kimataifa.


.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...