BODI ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) imeshiriki katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Jukwaa la Wasimamizi wa Taaluma ya Ukaguzi Afrika (African Forum of Independent Accounting and Auditing Regulators (AFIAAR) wa mwaka 2026, unaofanyika mjini Port Louis, Mauritius kuanzia tarehe 2 hadi 5 Juni 2026.
Katika Mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Prof. Siasa Mzenzi, alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa AFIAAR. Pamoja na Mkurugenzi Mtendaji, NBAA imewakilishwa na CPA Pius Maneno, Mkurugenzi Mtendaji Mstaafu wa NBAA na Makamu Mwenyekiti anayemaliza muda wake wa jukwaa hilo; CPA Winnington Makaka, Mkuu wa Sehemu ya Ubora wa Ukaguzi (AQR); pamoja na Magreth Kageya, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano cha NBAA.
Lengo la mkutano huo ni kuwakutanisha wasimamizi wa taaluma ya Uhasibu na Ukaguzi barani Afrika ili kujadili masuala mbalimbali yanayohusu taaluma hiyo, hususan hali ya ubora wa ukaguzi. Majadiliano hayo yanalenga kuimarisha ubora wa taarifa za ukaguzi wa makampuni, jambo litakalosaidia kukuza uchumi wa Afrika kwa kuongeza imani ya wawekezaji kupitia taarifa sahihi na za kuaminika za kifedha.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA na Makamu Mwenyekiti wa AFIAAR, CPA Prof. Siasa Mzenzi, alisema: “Mkutano huu ni muhimu kwa taasisi yetu na Tanzania kwa ujumla, kwani umetupatia fursa ya kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu mbinu bora za usimamizi wa taaluma ya ukaguzi. Maarifa haya yatasaidia kuboresha ubora wa huduma za ukaguzi nchini na hivyo kuongeza uaminifu wa taarifa za kifedha zinazotolewa na taasisi na makampuni mbalimbali.”
Mkutano wa AFIAAR unawakutanisha wadau mbalimbali wa usimamizi wa taaluma ya ukaguzi kutoka nchi mbalimbali za Afrika kwa lengo la kuimarisha ushirikiano, kubadilishana uzoefu na kujadili mikakati ya kuendeleza ubora wa ukaguzi barani humo.



.jpeg)
.jpeg)


.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...