-Agusia tamaa ya maisha inavyochochea biashara dawa za kulevya kwa vijana
-Ataka vyombo vya ulinzi na usalama kuchunguza wenye Show room
Na Said Mwishehe,Michuzi TV
MKUU wa Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam Sixtus Mapunda, amesema njia madhubuti ya kumaliza biashara ya dawa za kulevya nchini ni kukata cheni yote ya biashara hiyo kuanzia katika ngazi ya jamii ya kwenye mitaa huku akiitaka wananchi kushiriki mapambano dhidi ya dawa za kulevya.
Mapunda ametoa kauli hiyo leo Julai 23,2026 alipokuwa mgeni rasmi katika Tamasha laKufikia na kuhamasisha jamii dhidi ya madhara ya dawa za kulevya lililoandaliwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya(DCEA).
Amesema pamoja na juhudi za kudhibiti uzalishaji, usafirishaji na uhifadhi wa dawa za kulevya, hatua hiyo bado ni ngumu kutokana na mbinu mbalimbali zinazotumiwa na wahalifu, hivyo jamii inapaswa kuelekeza nguvu zaidi katika kuzuia matumizi ya dawa hizo.
"Siku tusipokuwa na watumiaji, maana yake tumeshakata cheni. Kwenye biashara yoyote demand ndiyo inaleta supply. Ukikata uhitaji, mzigo utakosa soko," amesema.
Amesema wazazi wana wajibu wa kuanza kuwapa watoto elimu kuhusu madhara ya dawa za kulevya tangu wanapoanza kupata ufahamu ili kuwajengea uwezo wa kukataa vishawishi vinavyoweza kuharibu maisha yao.
Aidha, amewatahadharisha vijana kutojaribu kutumia dawa za kulevya kwa kudhani ni fasheni au starehe, akieleza kuwa uraibu huanza taratibu lakini madhara yake huwa makubwa na wakati mwingine hushindikana kurekebishwa.
“Nilipotembelea banda la Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nimeoneshwa sampuli mbalimbali za dawa za kulevya ambazo zimetengenezwa kama keki ambazo zinazotumiwa na baadhi ya wanafunzi wa sekondari na vyuo vikuu katika sherehe binafsi.
“Tumefika katika hatua mbaya huko nyuma tulianza kama watumiaji baadae tukawa watumiaji na wasafirishaji lakini hivi sasa tumekuwa watengenezaji wa dawa za kulevya.Ni hatua mbaya sana na hivyo niwajibu wetu kukomesha dawa hizo kwa wote kushiriki katika mapambano.”
Amefafanua iwapo baadhi ya wanafunzi wa sekondari na vyuoni wameanza kutumia dawa za kulevya je hilo Taifa mbele ya safari bila kuchukua hatua hatma ya nchi itakuaje.
Katika hatua nyingine, amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuendelea kufuatilia mitandao inayohusishwa na biashara haramu ya dawa za kulevya pamoja na mifumo ya utakatishaji fedha, akisema baadhi ya maisha ya anasa yasiyoelezeka yanaweza kuwa yanawavutia vijana kuingia katika biashara hiyo.
Ametoa mfano katika mitandao ya kijamii kuna baadhi ya watu wanaweka video wakionesha fedha bila kueleza walikozitoa jambo ambalo linalotia shaka na walikozipata na wanafanya hivyo kama sehemu ya kuhamasisha vijana kuingia kwenye maisha ya Misheni Town.
“Nilishasema katika Wilaya ya Temeke ni marufu wananchi kuonesha fedha katika mitandao ya kijamii na nikibaini tu huyo aliyeonesha hiyo video atamakatwa akahojiwe alikotoa hizo fedha maana fedha iliyotafutwa kwa jasho huwezi kuonesha.
“Nilimkamata cha kwanza nitawaambia TRA wakate kodi yao na kisha Polisi wamuweke mahabusu kwa ajili ya usalama wake maana anakaribisha wezi mtaani kwake.Lakini nyuma ya hizi video kuna mazingira ya kuhamasisha vijana kuingia kwa lengo la kutafuta maisha rahisi na matokeo yake unaingizwa katika biashara haramu kama ya dawa za kulevya.”
Pia amesema kwasasa mtaani kumekuwepo na maeneo mengi ya kuuza magari tena yenye gharama kubwa akitoa mfano uwepo wa Show room maeneo ya Buza au Mbagala.”Unajiuliza nani anaweza kununua BMW Buza?
“Sio kwamba nawatuhumu hapana lakini inatia mashaka na vyombo vya ulinzi mnaweza kwenda kuzungumza nao kirafiki tu.Isije ikawa mtu anatumia biashara ya magari kutakatisha fedha ambazo zimetokana na dawa za kulevya.”
Pia amewataka wananchi kutoa taarifa kuhusu watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya badala ya kuwaficha, akisisitiza kuwa vita dhidi ya dawa za kulevya itafanikiwa pale jamii itakapokataa biashara hiyo kwa vitendo na si kwa maneno pekee.
Pamoja na hayo amesema mapambano dhidi ya dawa za kulevya yanahitaji ushirikiano wa serikali, wazazi, vijana na jamii kwa ujumla ili kulinda kizazi cha sasa na cha baadaye dhidi ya athari za janga hilo.




.jpeg)


.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...