Na Benny Mwaipaja, London.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amewakaribisha wawekezaji kutoka jumuiya ya kimataifa, kuchangamia fursa za uwekezaji nchini Tanzania katika sekta mbalimbali zikiwemo miundombinu, nishati, viwanda, kilimo, madini na huduma za kifedha.

Mhe. Balozi Omar ametoa wito huo jijini London nchini Uingereza alipoongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Kimkakati wa Uwekezaji na Ushirikiano wa Tanzania (Tanzania Strategic Investment and Partnership Forum) ukiwakutanisha viongozi wakuu wa taasisi kubwa za kifedha duniani, sekta ya bima na vihatarishi ulioandaliwa na Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Standard Bank ya nchini humo.

Alisema kuwa Serikali imeweka mazingira bora ya uwekezaji pamoja na vivutio vya kikodi ili kuvutia mitaji kutoka nje itakayochangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayoelekeza nchi ifikie uchumi wa dola za Marekani trilioni 1 ifikapo mwaka 2050 ambapo asilimia 70 ya fedha hizo zinatarajiwa kutoka sekta binafsi.

Awali, katika hotuba yake, Mhe. Balozi Omar aliwasilisha mwelekeo wa uchumi wa Tanzania chini ya Dira ya Maendeleo 2050, akibainisha kwamba uchumi wa Tanzania ulikua kwa asilimia 5.9 mwaka 2025, ukilinganisha na asilimia 5.5 mwaka 2024 huku Mfumko wa bei ukiendelea kubaki chini ya asilimia 5, miongoni mwa viwango vya chini zaidi barani Afrika;

Alisema kuwa nakisi ya bajeti imepungua hadi asilimia 3.1 ya Pato la Taifa; Karibu asilimia 74.2 ya bajeti ya Taifa sasa inagharamiwa na mapato ya ndani; Deni la Taifa linabaki himilivu kulingana na tathmini ya Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF.

Kwa upande wao, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Standard Bank Ulaya na Mkurugenzi Mtendaji wa Standard Bank Tanzania, Bwana Ian Carson, alisisitiza dhamira ya benki hiyo ya kuendelea kuunganisha Afrika na masoko ya fedha ya kimataifa, akiitaja Tanzania kuwa miongoni mwa maeneo bora zaidi barani Afrika kwa uwekezaji wa muda mrefu.

Akizungumza wakati wa Mkutano huo, Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mhe. Balozi Mbelwa Kairuki, alisema Serikali inaendelea kuwa na dhamira ya kudumisha mazungumzo ya mara kwa mara na jumuiya ya kimataifa ya wawekezaji.

"Tanzania inatekeleza mpango kabambe wa mageuzi ya kiuchumi unaojikita katika usimamizi imara wa uchumi mkubwa, mageuzi ya kimuundo na ushiriki wa sekta binafsi. Tunakaribisha ushirikiano endelevu na wawekezaji wa kimataifa kama washirika katika kufikia ukuaji wa uchumi endelevu na jumuishi," alisema Mhe. Balozi Kairuki.

Wawekezaji kadhaa walitaka ufafanuzi kuhusu mradi wa dola bilioni 42 wa Gesi Asilia Iliyogandamizwa (LNG) ambapo Mhe. Balozi Omar alieleza kuwa mazungumzo yamepiga hatua kubwa na masuala yaliyobaki ni ya ndani kati ya washirika wa kibiashara, huku Serikali ikiwa tayari kuendelea mara washirika hao watakapokamilisha michakato yao ya ndani.

Aidha, wawekezaji walionesha shauku kubwa kuhusu Reli ya Kisasa (SGR), Bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara, pamoja na njia za kibiashara za kikanda ambapo Serikali ilieleza kuwa ifikapo 2030/31, karibu kilomita zote 2,000 za mtandao wa SGR zitakuwa zimekamilika, hatua itakayoimarisha nafasi ya Tanzania kama lango kuu la kibiashara Afrika Mashariki.

Masuala mengine yaliyojadiliwa ni pamoja na upatikanaji wa fedha za kigeni, usalama wa nishati, uchumi wa kidijitali, kilimo na uongezaji thamani wa mazao kama pamba (mpango wa "Cotton-to-Cloth").

Mkutano huo, ambao ni sehemu ya jitihada endelevu za kidiplomasia za kiuchumi za Tanzania, uliongozwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Hamis Mussa Omar (Mb), akiambatana na Kamishna wa Usimamizi wa Deni la Serikali, Bwana Japhet Justine, huku Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza ukiwakilishwa na Mhe. Balozi Mbelwa Kairuki.


Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akizungumza wakati wa Mkutano wa Kimkakati wa Uwekezaji na Ushirikiano wa Tanzania (Tanzania Strategic Investment and Partnership Forum) uliowakutanisha viongozi wakuu wa taasisi kubwa za kifedha duniani, sekta ya bima na vihatarishi, ulioandaliwa na Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Standard Bank, Jijini London nchini Uingereza.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha-London).








Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...