Mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mke wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Salma Rashid Kikwete, tarehe 7 Julai 2026 aliongoza Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili yaliyofanyika katika Bunge la Uingereza (House of Lords), jijini London.

Maadhimisho hayo yalifanyika kwa mwaliko maalum wa Mheshimiwa Lord Paul Boateng, Mjumbe wa Baraza la Juu la Bunge la Uingereza (House of Lords), na yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali, wanadiplomasia, wabunge, wadau wa elimu pamoja na wapenzi wa lugha ya Kiswahili kutoka mataifa mbalimbali.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mheshimiwa Salma Kikwete alisisitiza umuhimu wa Kiswahili kama chombo cha kuimarisha mshikamano, utamaduni na maendeleo ya kijamii na kiuchumi barani Afrika na duniani kwa ujumla. Alieleza kuwa kuendelea kwa matumizi ya Kiswahili katika majukwaa ya kimataifa ni ushahidi wa nafasi yake kubwa katika kuunganisha watu wa tamaduni na mataifa mbalimbali.

Mheshimiwa Salma Kikwete, ambaye pia ni Balozi wa Heshima wa Kiswahili Barani Afrika, alibainisha kuwa lugha ya Kiswahili imeendelea kupata heshima na kutambulika duniani, hatua inayochangiwa na juhudi za viongozi, taasisi na wadau mbalimbali wanaoendelea kuikuza na kuieneza lugha hiyo katika nyanja za elimu, biashara, diplomasia na teknolojia.

Maadhimisho hayo pia yalihudhuriwa na Mabalozi wa nchi mbalimbali za Afrika nchini Uingereza wakiongozwa na Mheshimiwa Christiane Katsande, Balozi wa Zimbabwe nchini Uingereza na Amidi wa Mabalozi wa nchi za Afrika wanaowakilisha mataifa yao nchini humo. Ushiriki wa mabalozi hao uliakisi mshikamano wa Afrika katika kuendeleza na kuipa hadhi lugha ya Kiswahili kama nyenzo ya mawasiliano na utangamano wa bara hilo.

Kwa upande mwingine, maadhimisho hayo yalipambwa pia na uwepo wa mwanamuziki maarufu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kanda Bongo Man, ambaye ni miongoni mwa wasanii wa Afrika waliotoa mchango mkubwa katika kueneza matumizi na umaarufu wa Kiswahili kupitia muziki wake uliovuka mipaka ya bara la Afrika na kufikia hadhira ya kimataifa.

Aidha, Mheshimiwa Salma Kikwete aliipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na wadau wengine kwa juhudi zao za kuendeleza na kuhamasisha matumizi ya Kiswahili kimataifa, akisisitiza kuwa lugha hiyo ni sehemu muhimu ya urithi wa Afrika na nyenzo ya kuimarisha ushirikiano wa kimataifa.

Maadhimisho hayo yaliyofanyika katika Bunge la Uingereza yameendelea kuonesha kukua kwa hadhi na ushawishi wa Kiswahili duniani, huku Tanzania ikiendelea kuwa kinara katika juhudi za kukuza na kueneza lugha hiyo katika ngazi ya kimataifa.









Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...