📍Ni baada ya MwanaFA kutoa fedha za kugharamia matibabu hayo


MUHEZA:

MBUNGE wa Muheza na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma, maarufu kama 'MwanaFA', ametekeleza ahadi yake kwa kutoa chupa 99 za dawa ya kutibu sumu ya nyoka (antivenom) zenye thamani ya shilingi milioni 15, ili ziweze kutolewa bure kwa wananchi.

Mhe. Mwinjuma amekabidhi dawa hizo Julai 24, wakati wa kikao cha ndani cha wana CCM wa Kata za Tongwe na Nkumba, na kueleza kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa wakati wa kampeni mwaka jana.

"Mganga Mkuu, niliahidi kwamba endapo wananchi wa Muheza watanichagua tena, dawa za sumu ya nyoka nitazitoa ili wananchi watibiwe bure. Leo nakukabidhi chupa hizi 99 zenye thamani ya shilingi milioni 15," alisema Mhe. Mwinjuma.

Wilaya ya Muheza, yenye jumla ya vijiji 126 na kata 37, imezungukwa na mazingira ya misitu ambayo hupelekea wananchi kung'atwa na nyoka mara kwa mara wanapokuwa katika shughuli zao za mashambani.

Akithibitisha ukubwa wa tatizo hilo wakati akipokea dawa hizo, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Dkt. Fani Mussa, alisema kwa mwaka 2024/25 pekee, jumla ya watu 108 waliripotiwa kung'atwa na nyoka, huku watu 13 kati yao wakifariki dunia.

"Tunakushukuru mbunge kwa dawa hizi, umewasaidia sana wananchi wetu hapa wilayani kufuatia kilio chao cha muda mrefu. Tutazisambaza katika vituo vyetu vya afya na zahanati na wananchi watakaoumwa na nyoka watatibiwa bure kuanzia sasa," alisema Dkt. Fani.

Inaelezwa kuwa dozi moja ya dawa hiyo inagharimu kati ya shilingi 293,000 hadi 300,000, kiwango ambacho ni kikubwa kwa wananchi wengi wa kawaida kuweza kikumudu kutokana na ugumu huo, waathirika wengi walikuwa wakilazimika kukimbilia kwa waganga wa kienyeji.

Akizungumzia msaada huo, Katibu wa CCM Wilaya ya Muheza, Simon Leng'ese, alimshukuru mbunge huyo na kumwelezea kama kiongozi mwenye utu na anayejali maisha ya wapiga kura wake.

"Mheshimiwa mbunge, kwa niaba ya CCM tunakupongeza sana. Si watu wote wenye moyo kama huo, lakini kwa kitendo hiki cha kutoa dawa, umetenda jambo kubwa ambalo Mungu tu atakulipa. Sisi wenzako wa Muheza tutahakikisha tunakuunga mkono kwa sababu wewe ni hazina ya Muheza na Taifa kwa ujumla," alisema Leng'ese.

Kwa upande wake, mmoja wa wananchi kutoka Kijiji cha Nkumba Stuart Mdachi aliyehudhuria kikao hicho, alipongeza hatua hiyo na kukiri kuwa imekuja wakati mwafaka.

"Kiukweli mbunge tuliyenaye, hiki alichofanya ni jambo kubwa sana. Wananchi wengi walikuwa wakishindwa kwenda hospitali kwa sababu walikuwa hawana shilingi laki tatu, hivyo wanaenda kwa waganga wa kienyeji au kutumia dawa za mitishamba na wakati mwingine kupoteza maisha," alisema mwananchi huyo.





Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...