Njedengwa - Dodoma 📍

SERIKALI inaendelea na utekelezaji wa mkakati wake wa kuongeza tija katika kilimo baada ya kusambaza pampu za Umwagiliaji kwa vikundi vya wakulima na kuchimba visima 390 katika mikoa 15, hatua inayotarajiwa kuwawezesha wakulima kulima mwaka mzima na kuongeza uzalishaji wa mazao.

Hatua hiyo itawanufaisha wakulima 15,022 kupitia vikundi 769, huku eneo la ekari 13,518.75 likitarajiwa kuingia kwenye kilimo cha umwagiliaji na kupunguza utegemezi wa mvua.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), Raymond Mndolwa, alisema pamoja na Tume kuendelea na ujenzi wa miradi ya Umwagiliaji na ile ya kimkakati pia inaendelea kutekeleza kwa vitendo mkakati wake wa kuongeza tija katika kilimo kwa kusambaza pampu za Umwagiliaji kwa vikundi vya wakulima na kuchimba visima 390 katika mikoa 15.

Hatua hiyo inatarajiwa kuwawezesha wakulima kulima mwaka mzima na kuongeza uzalishaji wa mazao.

Alisema, mpango huo unatekeleza maelekezo ya Serikali ya kuwawezesha wakulima wenye mashamba madogo kujikwamua kiuchumi hususani wanawake na vijana kwa kupata uhakika wa maji.

"Tumeelekezwa kutafuta njia zitakazowawezesha wananchi wa kipato cha chini kujiongezea kipato. Ndiyo maana pamoja na miradi mikubwa ya Umwagiliaji, tumeanza uchimbaji wa visima na ugawaji wa pampu kwa wakulima wadogo," alisema.

Alisema pampu hizo ni maalumu kwa wakulima wanaolima karibu na mito na maziwa ili kuwasaidia kufanya kilimo kinachohifadhi mazingira na kuongeza uzalishaji.

Mndolwa alisema kati ya pampu 2,000 zilizonunuliwa na Serikali, pampu 1,000 tayari zimepokelewa na kupelekwa katika mikoa ya Mwanza, Mara, Kagera, Kigoma, Simiyu, Geita na Katavi kwa ajili ya kuanza kutumika.

Alisema pampu hizo zitagawiwa kwa vikundi 769 vya wakulima na kunufaisha wanawake 6,335 na wanaume 8,702, hivyo kufikisha jumla ya wanufaika 15,022.

"Pampu hizi zitawasaidia wakulima kuondokana na utegemezi wa mvua na kuwawezesha kulima misimu yote ya mwaka, jambo litakaloongeza uzalishaji na kipato chao," alisema.

Mndolwa alisema hadi sasa Tume imechimba visima 390 katika mikoa 15, ambapo Dodoma inaongoza kwa visima 93, ikifuatiwa na Manyara na Tabora zenye visima 44 kila mmoja, Geita 42, Singida 32, Njombe 30, Tanga 22, Iringa 20, Mara na Morogoro visima 17 kila mmoja.

Alitaja mikoa mingine iliyonufaika ni Pwani na Arusha zenye visima 10 kila mmoja, Mtwara nane, Mbeya saba na Ruvuma visima vitano.

Alisema Serikali pia imeanza ununuzi wa pampu 500 kwa ajili ya visima hivyo, ambapo pampu 100 tayari zimepokelewa, nyingine 100 ziko njiani kutoka kwa mtengenezaji na pampu 300 zipo katika hatua za manunuzi.

Mbali na pampu hizo, alisema Serikali inatarajia kupokea pampu nyingine 1,000 zinazotumia nishati ya jua ambazo zitasambazwa katika maeneo yenye changamoto ya upatikanaji wa umeme ili kuongeza wigo wa kilimo cha umwagiliaji.

Alifafanua kuwa visima vinachimbwa kwenye mashamba ya wakulima baada ya kuunganishwa katika vikundi, lakini hubaki kuwa mali ya umma ili wanakikundi wote wanufaike kwa usawa na kuhakikisha huduma hiyo inadumu.

Aidha, alisema vikundi vyote vinavyonufaika husajiliwa kwa mujibu wa sheria ili kurahisisha usimamizi wa miradi hiyo pamoja na ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

Mndolwa alisema utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa pia kutoa ajira kwa zaidi ya vijana 4,000 watakaoshiriki katika ufungaji, uendeshaji na usimamizi wa mifumo ya Umwagiliaji, huku akisisitiza kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha Umwagiliaji unakuwa chachu ya mapinduzi ya kilimo, usalama wa chakula na ukuaji wa uchumi wa wananchi.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...