MAHAKAMA ya Rufani Tanzania imetupilia mbali ombi la Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) lililotaka kuruhusiwa kuwasilisha ushahidi wa nyongeza katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, na hivyo kuacha uamuzi wa Mahakama Kuu ukiwa palepale.
Uamuzi huo ulitolewa na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani lililoundwa na Jaji Augustine Mwarija, Jaji Zahara Muruke na Jaji Amour Khamisi, ambao walikubaliana na uamuzi wa awali wa Mahakama Kuu uliotolewa na Jaji Dunstan Ndunguru, akisaidiana na Majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.
Akisoma hukumu, Jaji Mwarija alisema hoja kuu ilikuwa kubaini kama Mahakama Kuu ilikosea kwa kujadili na kukataa notisi ya ushahidi wa nyongeza bila kuipa Jamhuri nafasi ya kusikilizwa, lakini Mahakama ya Rufani ilibaini kuwa upande wa mashtaka ulipewa fursa ya kutosha kueleza msimamo wake.
Mahakama ilieleza kuwa notisi ya Jamhuri ililenga kuongeza maelezo ya ushahidi wa ACP Amini Mahamba kuhusu uchunguzi wa matukio ya Oktoba 29, 2025, maelezo ambayo hayakusomwa wakati wa mwenendo wa kupeleka shauri Mahakama Kuu (committal proceedings).
Hata hivyo, Lissu alipinga hatua hiyo akidai kuwa kifungu cha 308 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai hakiruhusu kuwasilishwa kwa ushahidi mpya kutoka kwa shahidi ambaye tayari ushahidi wake ulishawasilishwa wakati wa committal, bali kinahusu mashahidi ambao taarifa zao hazikusomwa kabisa.
Mahakama ya Rufani ilikubaliana na tafsiri hiyo, ikisema kifungu hicho kinatoa nafasi ya kumwita shahidi ambaye taarifa yake haikusomwa wakati wa committal, lakini hakitoi mamlaka ya kumrejesha shahidi aliyekwisha kutoa ushahidi ili kuongeza ushahidi mpya alioupata baadaye.
Kutokana na tafsiri hiyo, Mahakama ilisema notisi ya Jamhuri ilikuwa imewasilishwa kwa msingi usio sahihi wa kisheria na kwamba Mahakama Kuu ilikuwa sahihi kuifuta kwa kuwa haikukidhi matakwa ya kifungu cha 308 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Katika uamuzi huo, Mahakama pia ilikataa ombi la Lissu la kulipwa fidia kwa madai ya kukaa mahabusu kwa siku 139 kutokana na kusimamishwa kwa mwenendo wa kesi wakati maombi hayo yalipokuwa yakisikilizwa.
Jaji Mwarija alisema Mahakama ya Rufani haina mamlaka ya kushughulikia ombi hilo kwa kuwa si Mahakama ya kwanza kusikiliza shauri, akifafanua kuwa fidia ya aina hiyo inaweza kutolewa tu endapo mshtakiwa ataachiwa huru na kubainika kuwa shtaka lilikuwa la kipuuzi au la kumsumbua bila sababu.
Kutokana na sababu hizo, Mahakama ya Rufani ilihitimisha kuwa ombi la DPP halikuwa na msingi wa kisheria na hivyo likatupiliwa mbali, hatua inayomaanisha uamuzi wa Mahakama Kuu wa kuzuia kuwasilishwa kwa ushahidi huo wa nyongeza unabaki kuwa halali.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...