Na Janeth Raphael - MichuziTv 

Matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini yanatarajiwa kuongezeka kwa kasi endapo wananchi wataendelea kupata taarifa sahihi, zinazoeleweka na zinazotolewa kwa ujumbe mmoja kutoka kwa wadau mbalimbali wanaohusika na sekta hiyo.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia,  Nolasco Mlay, wakati wa ufunguzi wa Warsha ya Kuwajengea Uwezo Waandishi wa Habari na Maafisa Mawasiliano wa Serikali kutoka mikoa, wizara, taasisi na mashirika yaliyo chini ya Wizara ya Nishati kuhusu uandishi na uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia. Warsha hiyo imefanyika Julai 14, 2026 mkoani Morogoro.

 Mlay amesema utoaji wa ujumbe sahihi na wenye uelewa wa pamoja ni nyenzo muhimu katika kuwasaidia wananchi kufanya maamuzi sahihi kuhusu matumizi ya teknolojia mbalimbali za nishati safi ya kupikia, ikiwemo gesi ya kupikia (LPG), umeme, biogesi, gesi asilia na mkaa mbadala.

Amesema Serikali inaendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wenye lengo la kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2034, angalau asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia.

Kwa mujibu wa Mlay, baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuzindua Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia mwaka 2024, Serikali iliendelea kuimarisha juhudi hizo kwa kuzindua Mkakati wa Mawasiliano mwaka 2025, unaolenga kuhakikisha ujumbe unaotolewa kwa wananchi kuhusu nishati safi ya kupikia unakuwa wa pamoja, sahihi na unaoeleweka.

Ameeleza kuwa mkakati huo unalenga kuwawezesha wadau wote wanaotoa elimu kwa umma kuwa na uelewa unaofanana ili kuondoa taarifa zinazokinzana, kuongeza uhamasishaji na kuwafanya wananchi kuchagua matumizi ya nishati safi kwa manufaa ya afya zao, mazingira na maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

 Mlay amesisitiza kuwa vyombo vya habari vina nafasi ya kipekee katika kufanikisha ajenda hiyo ya kitaifa, kwani vina uwezo mkubwa wa kufikisha ujumbe kwa mamilioni ya Watanzania na kuongeza uelewa kuhusu faida za matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Aidha, amewataka waandishi wa habari pamoja na Maafisa Mawasiliano wa Serikali kuendelea kuandika na kusambaza taarifa zenye usahihi, zinazozingatia ujumbe wa pamoja na zinazohamasisha mabadiliko ya tabia, akibainisha kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza upotoshaji, kuongeza uelewa wa jamii na kuharakisha utekelezaji wa malengo ya taifa ya matumizi ya nishati safi ya kupikia.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...