Na Mwandishi wetu, Mirerani
MWENGE wa uhuru umekagua na kutembelea mradi wa viti 120 na meza 120 za wanafunzi wa shule ya sekondari Tanzanite ya Kata ya Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.
Mkuu wa shule ya sekondari Tanzanite, Jude Samwel Mziray ameeleza hayo wakati akisoma taarifa ya mradi huo kwa kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru mwaka 2026 Wazo Mwang'onda.
Mwalimu Mziray amesema shule ya sekondari Tanzanite ilipokea viti na meza hizo Mei 28, mwaka 2026.
Amesema shule hiyo ilipokea viti 120 na meza 120 kwa ajili ya maandalizi ya kuwapokea wanafunzi wa kidato cha kwanza 2028 watakaohitimu darasa la sita na la saba kwa wakati mmoja 2027.
"Mradi huu umezingatia kigezo namba 53 cha namna Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro ilivyoandaa miundombinu ya kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2028," amesema.
Amesema mradi huo umetengewa kiasi cha shilingi 10,800,000.00 kutoka katika mapato ya Halmashauri ya Wilaya na fedha iliyotumika ni shilingi 10,560,000.00
"Ndugu kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa mradi huu umetekelezwa kwa kutumia mfumo wa kielektroniki wa manunuzi ya Taifa (NaST) na fundi aliyetengeneza viti 120 na meza 120 ni Ibrahim Elias Mmary.
Amesema mafanikio ya mradi huo wa viti na meza ni kupunguza idadi ya wanafunzi wasiokuwa na viti na meza watakaoingia kidato cha kwanza 2028 na vyumba vitatu kuanza kutumika.
"Tunaishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha mazingira ya kujisomea na kujifunzia katika shule hii," amesema mwalimu Mziray.
Hata hivyo, kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa mwaka 2026 amepongeza mradi huo ambao utakuwa na manufaa makubwa kwa wanafunzi hao.
Mwang'onda amewaasa wanafunzi wa shule hiyo watakaotumika madawati na meza hizo kuzitunza ili waweze kutumia kwa muda mrefu.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...