Sekta ya mifugo nchini inatarajiwa kuingia katika hatua mpya ya utoaji wa huduma kufuatia kuanzishwa kwa zana za kidijitali za Mfumo wa Ulezi wa Kitaaluma kwa Maduka ya Dawa za Mifugo (Agrovet Mentoring Framework–AMF) na Mfumo wa Ulezi wa Kitaaluma kwa Watoa Huduma za Afya ya Mifugo (Animal Health Mentoring Framework–AHMF), ambazo zinalenga kuongeza ubora, uwajibikaji na weledi katika sekta hiyo.
Akizungumza katika kikao cha wadau kilichowakutanisha taasisi mbalimbali za sekta ya mifugo Jijini Dodoma, Msajili wa Baraza la Madaktari wa Mifugo Tanzania, Dkt. Amani Kilemile, alisema mfumo wa sasa unaotumia nyaraka za karatasi katika kufuatilia na kusimamia wataalamu wa mifugo pamoja na wahudumu wa maduka ya dawa za mifugo umekuwa ukikabiliwa na changamoto mbalimbali, zikiwemo ugumu wa kufuatilia utendaji wa wataalamu, kuhifadhi kumbukumbu sahihi na kusimamia uzingatiaji wa viwango vya taaluma.
Alisema matumizi ya zana hizo za kidijitali yatamwezesha mlezi wa kitaaluma kufanya tathmini ya umahiri wa mtaalamu kwa wakati halisi, kurekodi maendeleo yake na kutoa mrejesho wenye muundo unaoeleweka, hatua itakayoongeza uwajibikaji na kuboresha ubora wa huduma zinazotolewa kwa wafugaji.
Dkt. Kilemile aliongeza kuwa tofauti na mfumo wa awali wa karatasi, zana hizo zitamwezesha mlezi kushuhudia utendaji wa kila siku wa mtaalamu, kubaini mapungufu ya uwezo, kutoa mafunzo ya vitendo na kufuatilia maendeleo yake kwa karibu ili kuhakikisha viwango vya kitaaluma vinaendelea kuzingatiwa.
Alisema mifumo hiyo pia itasaidia kusimamia maeneo muhimu ikiwemo uzingatiaji wa sheria na kanuni za taaluma, utoaji bora wa huduma kwa wateja, usambazaji unaowajibika wa dawa za mifugo, usimamizi wa stoo za dawa na bidhaa za mifugo pamoja na kuimarisha maadili ya taaluma.
Zana hizo zimetengenezwa na Brooke East Africa, shirika la ustawi wa wanyama lenye makao yake nchini Kenya, na zinatekelezwa nchini Tanzania na INADES-Formation Tanzania kwa kushirikiana na Arusha Society for Protection of Animals (ASPA), kwa lengo la kujenga uwezo wa wataalamu wa afya ya mifugo na wahudumu wa maduka ya dawa za mifugo.
Kwa upande wake, Wizara inayosimamia sekta ya mifugo ilieleza kuwa mfumo huo wa kidijitali utarahisisha ukusanyaji na uchambuzi wa taarifa, kuongeza ufanisi wa usimamizi na kuwezesha maamuzi yanayotegemea ushahidi, tofauti na mfumo wa karatasi ambao umekuwa ukisababisha ucheleweshaji wa taarifa na changamoto za ufuatiliaji.
Mkurugenzi Mtendaji wa INADES-Formation Tanzania, Bi. Jacqueline Nicodemus, pamoja na wawakilishi wa ASPA na Brooke East Africa, walisisitiza dhamira yao ya kuendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha mifumo hiyo inatekelezwa kwa ufanisi ili kuleta mageuzi katika sekta ya mifugo.
Wadau walieleza matumaini kuwa matumizi ya mifumo ya AMF na AHMF yataongeza uwezo wa wataalamu wa mifugo, kuboresha afya na ustawi wa wanyama, kuongeza uzalishaji wa mifugo, kuhamasisha matumizi sahihi ya dawa za mifugo na kujenga imani zaidi kwa wafugaji kupitia huduma zenye ubora, weledi na uwajibikaji.


.jpeg)
.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...