MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imeweka rekodi mpya katika ukusanyaji wa mapato baada ya kukusanya jumla ya Shilingi trilioni 37.96 katika mwaka wa fedha 2025/26, sawa na asilimia 105.24 ya lengo la kukusanya Shilingi trilioni 36.07.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, leo Julai 04, 2026 imeeleza kuwa mafanikio hayo katika makusanyo ya kodi ni sawa na ukuaji wa asilimia 17.61 ikilinganishwa na makusanyo ya Shilingi trilioni 32.27 yaliyopatikana katika mwaka wa fedha 2024/25.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa mafanikio hayo yametokana na kuendelea kutumia mbinu za kisasa katika usimamizi wa kodi, kuimarisha uzingatiaji wa sheria za kodi pamoja na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

Takwimu zinaonyesha kuwa katika miezi yote 12 ya mwaka wa fedha uliomalizika Juni 2026, TRA ilifanikiwa kuvuka malengo ya makusanyo ambapo kwa Mwezi Juni wameweka rekodi mpya kwa kukusanya Shilingi trilioni 4.01, sawa na ufanisi wa asilimia 107.98, huku Januari, Machi na Aprili pia zikifanya vizuri kwa kuvuka malengo yaliyowekwa.

Katika taarifa hiyo, TRA imeeleza kuwa mafanikio hayo yameiwezesha mamlaka hiyo kuweka rekodi mpya nne katika usimamizi wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali nchini, hatua inayodhihirisha kuendelea kuimarika kwa mifumo ya kodi na usimamizi wa mapato.

Mamlaka hiyo imewahakikishia wananchi na wadau mbalimbali kuwa itaendelea kuboresha huduma kwa walipakodi, kuimarisha matumizi ya teknolojia na kuhakikisha mapato ya Serikali yanaongezeka kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na utoaji wa huduma za kijamii.

Mafanikio ya TRA yanatarajiwa kuongeza uwezo wa Serikali kutekeleza bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27 kupitia mapato ya ndani, sambamba na kupunguza utegemezi wa misaada na mikopo ya nje.

TRA yavunja rekodi ya makusanyo kwa miaka miwili mfululizo mbali na kuvuka malengo ya makusanyo kwa miaka miwili mfululizo, TRA pia imeweka rekodi mpya ya kukusanya mapato kwa miezi 24 mfululizo kuanzia Julai 2024 hadi Juni 2026, ikiwa ni mara ya kwanza katika historia ya mamlaka hiyo.

Katika kipindi hicho, wastani wa ufanisi wa makusanyo umefikia asilimia 104.64.

Aidha, mwezi Desemba 2025 uliweka historia mpya baada ya TRA kukusanya Shilingi trilioni 4.13 ndani ya mwezi mmoja, kiwango kilichovunja rekodi ya awali ya Shilingi trilioni 3.58 iliyowekwa Desemba 2024.

Kwa mwaka wa fedha 2025/26, wastani wa makusanyo ya kila mwezi umefikia Sh. trilioni 3.16, kutoka wastani wa Sh.trilioni 2.69 uliopatikana mwaka 2024/25.

Mafanikio hayo yameelezwa kuwa yametokana na uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameendelea kusimamia mageuzi ya ukusanyaji wa mapato kwa kusisitiza utii wa sheria za kodi, kuhamasisha ulipaji wa hiari, kupanua wigo wa walipakodi, kuimarisha matumizi ya mifumo ya TEHAMA na kuhakikisha kodi zinazokusanywa zinatumika katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na utoaji wa huduma kwa wananchi.

Katika kipindi hicho, TRA imekamilisha ujenzi wa Mfumo wa Usimamizi wa Kodi za Ndani (IDRAS), ulioanza kutumika rasmi Februari 2026. Mfumo huo umeunganishwa na mifumo ya taasisi 52 za umma na taasisi 30 binafsi, hatua inayolenga kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato na kurahisisha utoaji wa huduma kwa walipakodi.

Vilevile, kampeni za kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari zimeendelea kuzaa matunda, ambapo kiwango cha utii wa walipakodi kimeongezeka kutoka asilimia 77.48 mwaka 2020/21 hadi asilimia 85.71 mwaka 2024/25, huku pengo la kodi likipungua hadi asilimia 1.89.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, utekelezaji wa sera za kiuchumi zinazolenga kuhimili misukosuko ya uchumi duniani umechangia kuongezeka kwa shughuli za uzalishaji na biashara nchini, hali iliyowezesha TRA kufikia ufanisi wa makusanyo wa wastani wa asilimia 105.24 katika mwaka wa fedha 2025/26, sambamba na ukuaji wa mapato wa asilimia 17.61.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...