Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
TAASISI zinazojihusisha na sekta ya ubaharia zimetakiwa kuimarisha ushirikiano ili kuwawezesha wanafunzi wanaohitimu masomo ya ubaharia kupata ajira kwenye meli mbalimbali na kuchangia ukuaji wa sekta hiyo nchini.
Wito huo umetolewa leo Julai 4, 2026 na Kiongozi wa Taasisi ya Mission for Seafarers, Father Johnson Lameck, wakati wa maadhimisho ya Siku Maalumu ya Kuwakumbuka na Kuwaombea Dua Mabaharia waliotangulia mbele za haki.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Father Lameck alisema Tanzania imejaliwa kuwa na bahari pamoja na fursa nyingi za uchumi wa buluu, hivyo kuna umuhimu wa taasisi zinazohusika na sekta ya ubaharia kushirikiana katika kuwaandaa wahitimu na kuwaunganisha na soko la ajira.
“Hapa nimesikia zipo taasisi mbalimbali. Tuone namna gani tunaweza kushirikiana na wanaosomesha mabaharia na kuwapatia vyeti. Kazi zao ni za meli na shughuli nyingine mbalimbali,” alisema.
Alisema kuna haja ya taasisi hizo kushirikiana na Chuo cha Mabaharia Dar es Salaam (DMI) ili wanafunzi wanaomaliza masomo wapate nafasi za ajira kwenye meli mbalimbali.
“Tuone namna gani tunaweza tukajikondesha na DMI ili wanafunzi hawa wanaomaliza waweze kupata ajira kwenye meli hizo. Hicho ndicho kilio chao kikubwa pale kwetu. Tunafahamu na tunaangalia namna gani tunaweza kusaidia wakapata ajira kwenye meli mbalimbali,” alisema.
Aidha, aliwataka viongozi wa taasisi mbalimbali kuweka mikakati ya pamoja ya kuwawezesha vijana kupitia miradi mbalimbali itakayochochea maendeleo yao na kuimarisha sekta ya ubaharia.
Pia alisisitiza kuwa sekta ya uchumi wa buluu ina fursa kubwa za ajira na maendeleo, akihimiza vijana kuzitumia rasilimali za bahari kujijengea uchumi na kuchangia maendeleo ya taifa.
Kwa upande mwingine, Father Lameck alitoa salamu za pole kwa familia zilizopoteza wapendwa wao baharini na kuwataka Watanzania kuendelea kuwaombea ili wapate faraja na nguvu wanapoendelea kuwakumbuka waliotangulia mbele za haki.



.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...