Na Avila Kakingo
CHUO Kikuu cha Aga Khan kupitia Taasisi ya Maendeleo ya Elimu Afrika Mashariki (IED, EA), kimewakutanisha waelimishaji wa walimu, watunga sera, watafiti, viongozi wa shule, washirika wa maendeleo, walimu wanafunzi na wataalamu wa elimu kutoka Afrika Mashariki na maeneo mengine kujadili mustakabali wa uandaaji wa walimu.

Mkutano huo wenye kaulimbiu “Kufikiria Upya Uandaaji wa Walimu: Mabadilishano ya Kujifunza Afrika Mashariki kuhusu Ubunifu na Utendaji”, unalenga kutoa jukwaa la kubadilishana uzoefu, kuchunguza mbinu bunifu na kuandaa kwa pamoja suluhisho la kuimarisha uandaaji wa walimu. Akizungumza katika mkutano huo, Mkuu wa IED, EA, Profesa Jane Rarieya, amesema mustakabali wa elimu katika Afrika Mashariki hautegemei kuwa na walimu wa kutosha pekee, bali namna wanavyoandaliwa, kusaidiwa na kuwezeshwa katika taaluma zao.

Profesa Rarieya amesema mabadiliko ya elimu yanachochewa na matumizi ya teknolojia za kidijitali na akili bandia (AI), mabadiliko ya tabianchi, ongezeko la utofauti na ujumuishi pamoja na mabadiliko ya matarajio kuhusu elimu. Amesema mkutano huo unatoa fursa kwa wadau kujifunza kutoka kwa kila mmoja, kuimarisha ushirikiano kati ya shule, vyuo vikuu, jamii na mifumo ya elimu, na kutafakari upya namna ya kuwaandaa walimu kukabiliana na mahitaji ya madarasa ya sasa.

Mabadilishano hayo yanafanyika kwa mtazamo wa kujifunza kwa vitendo na kushirikishana uzoefu, kupitia vikao vya kubadilishana uzoefu, maabara za utekelezaji, madarasa maalumu, mijadala ya pande zote na majadiliano ya paneli. Kupitia vikao hivyo, washiriki wanajadili changamoto zinazofanana, kujifunza kutokana na mazingira mbalimbali na kujenga ushirikiano wa kuimarisha mifumo ya elimu katika ukanda huo.

Eneo jingine linalopewa kipaumbele ni kuwawezesha walimu kuwa na uwezo na uhuru wa kitaaluma wa kushiriki katika mageuzi ya elimu. IED, EA imeeleza kuwa kadri nchi zinavyoendelea kutumia mitaala inayozingatia umahiri, walimu wanahitaji kuwa na uwezo wa kuelewa mahitaji ya wanafunzi, kufanya maamuzi sahihi ya kitaaluma, kutathmini ujifunzaji, kubadilisha mbinu za ufundishaji na kushirikiana na jamii wanazozihudumia.

Kwa mujibu wa IED, EA, mabadilishano hayo ni wito kwa walimu, serikali, vyuo vikuu, shule, jamii na washirika wa maendeleo kushirikiana katika kufikiria upya uandaaji wa walimu Afrika Mashariki. Hatua zinazopendekezwa ni pamoja na kuimarisha mafunzo ya vitendo na ulezi kwa walimu wanafunzi, kujenga jumuiya za kujifunza kitaaluma kwa walimu wanaoanza kazi na kuwapa walimu wenye uzoefu nafasi ya kuwa viongozi, walezi na washiriki katika ubunifu na tafiti za elimu.
Kwa upande wake, Mhadhiri wa Taasisi hiyo, Dkt. Nipael Mrutu, amesema kongamano hilo linalenga kutafakari aina ya mwalimu anayehitajika katika dunia inayobadilika kwa kasi.

Dkt.Mrutu amesema fursa hiyo inawawezesha wataalamu kubadilishana uzoefu kuhusu mbinu mbalimbali za ufundishaji, kutathmini zilizofanikiwa na ambazo hazikutoa matokeo yaliyotarajiwa na kutafuta njia bora za kuboresha elimu.

Amesema ubunifu ni muhimu kwa mwalimu wa sasa kwa kuwa anapaswa kutumia mbinu zinazowawezesha wanafunzi kujifunza kwa ufanisi na kukabiliana na mahitaji yanayobadilika katika jamii na dunia.

Naye mwalimu wa Shule ya Sekondari Jangwani na kiongozi wa Chama cha Walimu wa Somo la Kiingereza Tanzania, Ayub Msuya, amesema walimu wanapaswa kubadilisha mtazamo wa kuwalaumu wanafunzi wanaposhindwa kuelewa na badala yake kutafuta mbinu mpya zinazolingana na mahitaji yao.

Msuya amesema walimu wa Afrika Mashariki wanapaswa kujifunza kutoka kwa wenzao na kubadilishana mbinu za ufundishaji, ikiwamo matumizi sahihi ya teknolojia.

Amesema kwa somo la Kiingereza, walimu wanapaswa kuzingatia mazingira ya lugha wanamoishi wanafunzi na kuwajengea uwezo wa kuelewa, kuchambua na kutumia maarifa wanayopata.

Ameongeza kuwa kongamano hilo limefika wakati mwafaka kwa kuwa linawawezesha walimu kujifunza kutoka kwa wenzao wa nchi nyingine za Afrika Mashariki na kupata mbinu zitakazosaidia kuandaa wanafunzi wenye uwezo wa kuwasiliana, kuchambua na kutumia maarifa katika maisha ya sasa na yajayo.

Kwa mujibu wa Taasisi ya Maendeleo ya Elimu Afrika Mashariki, kongamano hilo pia linalenga kuimarisha ushirikiano kati ya walimu, serikali, vyuo vikuu, shule, jamii na washirika wa maendeleo katika kuboresha uandaaji wa walimu katika ukanda huo.

Kupitia mijadala ya vikundi, maabara za utekelezaji, madarasa maalumu, meza za majadiliano na mijadala ya pamoja, washiriki wanajadili namna ya kuimarisha mafunzo ya vitendo na malezi kwa walimu wanafunzi, kujenga jumuiya za kitaaluma kwa walimu wanaoanza kazi na kuwawezesha walimu wenye uzoefu kushiriki katika uongozi, utafiti na ubunifu wa elimu.



Matukio mbalimbali katika picha.
Picha ya pamoja
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...