Na Janeth Raphael – Michuzi TV
Watu wanane wamefariki dunia na wengine 66 kujeruhiwa kufuatia ajali mbaya iliyohusisha mabasi mawili ya abiria yaliyogongana uso kwa uso katika eneo la Ibihwa, Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, mkoani Dodoma.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Rehema Jeremia, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo, akieleza kuwa ilihusisha basi la Isamilo lenye namba za usajili T 428 EXP, lililokuwa likitoka Mwanza kuelekea Dar es Salaam, na basi la Libanika Luxury lenye namba za usajili T 897 DUP, lililokuwa likitoka Dar es Salaam kuelekea Mwanza.
Akizungumza baada ya kuwatembelea majeruhi waliolazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amesema watu saba walifariki dunia papo hapo eneo la tukio, huku mtu mmoja akifariki baadaye alipokuwa akipatiwa matibabu hospitalini, na kufanya idadi ya vifo kufikia wanane.
Senyamule amesema kati ya majeruhi 66, watu tisa wanaendelea kupatiwa matibabu wakiwa katika hali mbaya, huku majeruhi 57 wakiwa katika hali ya kuridhisha.
Ameongeza kuwa majeruhi wamepelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Hospitali ya Makole na Hospitali ya Wilaya ya Bahi, ambako wanaendelea kupatiwa huduma za matibabu.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa awali, chanzo cha ajali hiyo kinadaiwa kuwa ni dereva mmoja kujaribu kulipita gari lingine bila kuchukua tahadhari stahiki, hali iliyosababisha mabasi hayo kugongana uso kwa uso.
Mmoja wa majeruhi wa ajali hiyo, Jail Martin, amesema tukio hilo lilitokea majira ya saa 12:00 asubuhi baada ya basi walilokuwa wakisafiria kuanza kuyumba kabla ya kugongana uso kwa uso na basi lililokuwa likitokea upande wa pili wa barabara.
Jeshi la Polisi pamoja na vyombo vingine vya uokoaji vinaendelea na uchunguzi wa kina kubaini chanzo halisi cha ajali hiyo huku juhudi za kuwahudumia majeruhi zikiendelea.


.jpeg)
.jpeg)


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...