Chama Kikuu cha Ushirika Tandahimba na Newala (TANECU) kimetangaza mafanikio makubwa katika sekta ya korosho baada ya kufanikiwa kupata zaidi ya Sh bilioni 1.6 kupitia mauzo ya korosho kimataifa zilizoongezwa thamani katika kiwanda chake cha kubangua korosho, huku kikieleza kuwa kipo katika hatua za mwisho za kuanza ujenzi wa kiwanda cha pili Wilaya ya Tandahimba.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye Maonesho ya Kilimo Kitaifa Nanenane yanayoendelea Jijini Dodoma Agosti 2, 2026, Mwenyekiti wa TANECU, Karimu Hamis Chipola, alisema wamefika kwenye maonesho hayo kuonesha mafanikio ya wakulima na mchango wa ushirika katika kuongeza thamani ya mazao na kuwanufaisha wanaushirika.

Chipola alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwaunganisha wakulima kupitia maonesho ya Nanenane, akisema yamekuwa jukwaa muhimu la kuonesha ubunifu na mafanikio ya sekta ya kilimo nchini.

Alisema TANECU imefanikiwa kutekeleza kwa kiwango kikubwa maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 mazao yanayozalishwa nchini yanachakatwa na kuongezwa thamani ili kuongeza kipato cha wakulima.

“Tayari kiwanda chetu cha kubangua korosho kinafanya kazi na bidhaa zilizochakatwa zimeuzwa katika masoko ya kimataifa, ambapo tumepata zaidi ya shilingi bilioni 1.6. Hii ni hatua kubwa kwa wakulima wetu,” alisema Chipola.

Aliongeza kuwa maandalizi ya ujenzi wa kiwanda cha pili yamefikia hatua ya mwisho ya manunuzi, hatua ambayo itaongeza uwezo wa kuchakata korosho na kupanua masoko ya bidhaa za wakulima.

Katika kuboresha mfumo wa biashara ya korosho, Chipola alisema TANECU inaendelea kutekeleza maelekezo ya Wizara ya Kilimo kuhusu uuzaji wa korosho ghafi kupitia mfumo wa stakabadhi za ghala na Soko la Bidhaa Tanzania.

Pia alisema baada ya ziara ya Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, mkoani Mtwara, TANECU ilielekezwa kujenga maghala ya kuhifadhi korosho ili kupunguza gharama za usafirishaji kwa wakulima.

Kwa mujibu wa Chipola, wamepanga kujenga maghala sita, ambapo mawili tayari yamekamilika na yanatarajiwa kuzinduliwa Septemba 1, 2026, kabla ya kuanza kutumika katika msimu mpya wa mauzo ya korosho. Maghala manne yaliyobaki yataendelea kujengwa ili kukamilisha mpango huo.

Akizungumzia jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita, Chipola alisema serikali imeendelea kuwainua wakulima kupitia ruzuku ya pembejeo yenye thamani ya zaidi ya Sh trilioni 1.1.

Alisema TANECU imeunga mkono juhudi hizo kwa kuajiri maafisa ugani 13 waliopangiwa kufanya kazi katika wilaya za Tandahimba na Newala, ambapo wanatoa elimu ya matumizi sahihi ya pembejeo na mbinu bora za kilimo ili kuongeza uzalishaji.

Aidha, TANECU imejipanga kuendeleza kampeni ya “Linda Ushirika, Chagua Uadilifu”, iliyoanzishwa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, kwa kuendelea kutoa elimu kwa wakulima kuhusu umuhimu wa kulinda ushirika na kusimamia uwajibikaji.

Aliwahimiza wananchi wanaotembelea Maonesho ya Nanenane Jijini Dodoma kufika katika banda la TANECU kujionea bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na ushirika huo, hususan korosho zilizoongezwa thamani, pamoja na kupata elimu kuhusu kilimo na ushirika.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...