Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) umetangaza mpango wa kuongeza uzalishaji wa mbegu bora hadi kufikia tani 15,000 baada ya mavuno yanayotarajiwa hivi karibuni, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa mbegu bora kwa wakulima nchini.
Mtendaji Mkuu wa ASA, Mhandisi Innocent C. Masaka , ameyasema hayo Leo Agosti 1, 2026, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya Kilimo ya Nanenane jijini Dodoma ambapo hadi sasa wakala huo umezalisha tani 7,000 za mbegu, huku ukiendelea kuimarisha uzalishaji kupitia mashamba yake yaliyopo katika kanda mbalimbali za nchi na mahitaji ni kufikia Tani elfu 27.
Amesema ASA katika kuhakikisha wanaongeza uzalishaji wambegu wamejipanga kupanua ushirikiano na sekta binafsi kwa kuwapatia teknolojia za uzalishaji wa mbegu bora ili kuongeza kiwango cha uzalishaji na kuhakikisha wakulima wengi zaidi wanapata mbegu zenye ubora unaohitajika kwa wakati.
Mhandisi Masaka amesema mbegu zinazozalishwa na ASA zimeendelea kuonesha matokeo mazuri katika kanda zote za kilimo nchini, zikiwemo kusini, kaskazini, mashariki na magharibi, huku zikiwa na uwezo wa kuhimili ukame unaotokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Aidha, amewahimiza wakulima kutumia mbegu bora zilizothibitishwa na TOSCI ili kuongeza tija ya uzalishaji, amesema ASA imeendelea kuimarisha mfumo wa usambazaji kupitia mawakala, wasambazaji wakubwa na Wakala wa Huduma za Ugani Tanzania (NAESA), ambao huwafikishia wakulima teknolojia na mbegu bora kwa wakati.
Amewaalika wananchi kutembelea banda la ASA katika Maonesho ya Nanenane ili kujifunza kuhusu teknolojia za uzalishaji wa mbegu bora na huduma mbalimbali zinazotolewa na wakala huo kabla ya maonesho hayo kuhitimishwa Agosti 8, 2026.




Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...