Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa Umma na Mawasiliano wa Bodi ya Bima ya Amana (DIB) Lwaga Mwambande akizungumza na Waandishi wa habari kwenye Banda la DIB katika Maonesho ya Kilimo ya Kimataifa Nane Nane yanayoendelea kwenye Viwanja vya Dkt.John Samwel Malecela Nzuguni Jijini Dodoma.
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
BODI ya Bima ya Amana (DIB) imesema inaendelea kuchukua hatua za kuziimarisha taasisi za fedha zinazokabiliwa na changamoto za kifedha ili zisifilisike, hatua inayolenga kulinda amana za wananchi na kuzuia Serikali kutumia fedha nyingi kulipa fidia endapo taasisi hizo zitafungwa.
Akizungumza katika Maonesho ya Kilimo ya Kimataifa Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Samwel Malecela, Nzuguni jijini Dodoma, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa Umma na Mawasiliano wa DIB, Lwaga Mwambande, alisema moja ya majukumu ya bodi hiyo ni kusaidia taasisi za fedha zenye changamoto kwa kuzipa udhamini au mikopo maalumu ili ziweze kurejea katika hali ya kawaida ya uendeshaji.
Alisema hatua hiyo ni ya busara zaidi kuliko kusubiri taasisi hizo zifilisike na baadaye kutumia fedha nyingi kulipa fidia kwa waweka amana.
"DIB inalenga kuhakikisha taasisi za fedha zinaendelea kuwa imara huku haki za wananchi walioweka fedha zao zikiendelea kulindwa," alisema.
Mwambande aliwahakikishia wananchi kuwa fedha wanazoweka katika benki na taasisi za fedha zilizopewa leseni na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinalindwa kupitia mfumo wa Bima ya Amana.
Alifafanua kuwa mteja anapoanza kuweka fedha katika taasisi ya fedha yenye leseni ya BoT, amana yake huingia moja kwa moja katika mfumo wa kinga ya amana bila kulazimika kulipa gharama yoyote ya ziada.
Aidha, alisema kiwango cha juu cha fidia kinachotolewa kwa sasa ni Shilingi milioni 7.5 kwa kila mweka amana endapo benki itafungwa.
Alieleza kuwa mteja mwenye amana isiyozidi kiwango hicho hulipwa fedha zake zote, huku mwenye amana inayozidi kiwango hicho akilipwa kwanza kiwango kilichowekwa na kisha kuendelea kudai salio lililobaki kupitia mchakato wa ufilisi wa benki husika.
Mwambande alisema Mfuko wa Bima ya Amana unachangiwa na benki na taasisi zote za fedha zinazopokea amana kutoka kwa wananchi, ambapo kila taasisi huchangia asilimia 0.15 ya jumla ya amana zake kila mwaka.
Aliongeza kuwa fedha hizo huwekezwa katika dhamana za Serikali na maeneo mengine salama ya uwekezaji ili kuhakikisha mfuko unakuwa na uwezo wa kutosha kulipa fidia pale inapohitajika.
Pia alisema, pamoja na jukumu la kulipa fidia kwa waweka amana, DIB ina wajibu wa kusimamia ufilisi wa benki zinazofungwa. Kwa sasa bodi hiyo inaendelea kusimamia ufilisi wa benki tisa zilizofungwa katika nyakati tofauti, ikiwa na lengo la kukusanya mali za benki hizo na kuwalipa wadai, hususan wale wenye amana zinazozidi kiwango kinacholindwa na bima ya amana.


.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...