Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Udhibiti wa Mbegu za Kilimo Tanzania (TOSCI), Nyasebwa E. Chimagu, amesema mbegu za asili ni lazima ziwe na afya na ziwe chini ya utaratibu rasmi wa usimamizi ili kuhakikisha hazina magonjwa na zinaendelea kuhifadhiwa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Chimagu alitoa kauli hiyo Agosti 5, 2026, jijini Dodoma wakati akizungumza katika mkutano wa wadau wa kilimo ikolojia uliofanyika ndani ya Maonesho ya Kilimo ya Nanenane Kitaifa.

Alisema sheria ya mbegu nchini inaeleza wazi masharti ya usajili, ubora na usimamizi wa mbegu zinazozalishwa kwa ajili ya biashara bila kubagua aina yoyote ya mbegu, Aidha, alibainisha kuwa Tanzania imeanza hatua za awali za kuandaa sheria maalumu kufuatia Mkataba wa Kimataifa wa mwaka 2001, unaolenga kulinda haki za wakulima juu ya mbegu zao za asili pamoja na rasilimali za mimea.

Chimagu alisema nasaba za mimea ni rasilimali muhimu yenye mchango katika maendeleo ya sekta ya kilimo na uchumi wa nchi. Alieleza kuwa kupitia Wizara ya Kilimo na TOSCI, juhudi zimeendelea kufanyika katika kulinda nasaba hizo, huku changamoto kubwa zikitajwa kuwa ongezeko la idadi ya watu na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Alisisitiza kuwa ni muhimu kuhakikisha mbegu za asili zinapatikana kwa wingi ili wakulima wawe na uhuru wa kuchagua aina ya mbegu zinazokidhi mahitaji yao ya uzalishaji.

Kuhusu kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, Chimagu alisema TOSCI inaendelea kuwekeza katika tafiti za kina zinazolenga kulinda nasaba za mimea na kuboresha mbegu ili ziweze kustahimili mazingira yanayobadilika.

Akitoa mfano, alisema nchini Misri mkulima wa mahindi anaweza kuvuna tani 10 hadi 12 kwa hekta moja kutokana na matumizi ya mbegu bora na teknolojia sahihi, Alisema Tanzania inaendelea kushirikiana na Wizara ya Kilimo kuhakikisha mbegu za asili zinahifadhiwa na kupatikana ili wakulima wawe na uchaguzi wa aina ya mbegu kulingana na mahitaji yao.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mtandao wa Mashirika Yanayojishughulisha na Utunzaji wa Bionuai Tanzania (TABIO), Abdullah Ramadhan Mkindi, alisema taasisi hiyo inaendelea kuhamasisha uhifadhi na matumizi ya mbegu za asili pamoja na mifugo ya asili, ikiwemo ng’ombe na kuku wa kienyeji, ili rasilimali hizo zisiendelee kutoweka kutokana na mchango wake katika usalama wa chakula na uhifadhi wa mazingira.

Naye Mratibu wa Utafiti na Masuala ya Kisera kutoka Swiss Aid Tanzania, Gladness Martine, alisema taasisi hiyo imeshiriki mkutano huo kwa lengo la kushirikisha uzoefu kuhusu umuhimu wa tafiti shirikishi zinazowawezesha wakulima kuhifadhi, kulinda na kuendeleza matumizi ya mbegu za asili kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho. 





Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...