Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) kimeonyesha ubunifu katika teknolojia, upangaji wa ardhi na ujasiriamali, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kutumia elimu na tafiti kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
Akizungumza Agosti 19, 2026, katika Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu inayoendelea Jijini Tanga, Mkuu wa Chuo Cha Mipango Profesa Hozen Mayaya, amesema chuo hicho kimekuja kuonyesha bunifu mbalimbali zinazofanywa na wanafunzi ili kuisaidia jamii.
Amesema chuo hicho kina kampasi mbili ambazo ni Dodoma na Mwanza, na kinafundisha vijana masuala ya TEHAMA , ambapo baadhi yao mwanafunzi amebuni mfumo unaolenga kusaidia kuboresha huduma katika sekta ya afya na Benki kwa kuondoa foleni na kumsaidia mteja kufahamu muda wa kupata huduma na kuondoa upendeleo.
Aidha, ameeleza kuwa wanatoa mafunzo ya upangaji wa ardhi, miji na vijiji, akisisitiza umuhimu wa kuwaandaa wataalamu watakaokabiliana na changamoto za ukuaji wa makazi.
“Tunafundisha masuala ya upangaji miji pamoja na upangaji wa vijiji, kwa sababu tunaamini vijiji vya leo ni miji ya kesho,” amesema.
Amesema kupitia programu ya Mipango Planning, Entrepreneurship and Innovation Centre MEI wanafunzi wanapata fursa ya kutumia maarifa wanayopata darasani kutengeneza bidhaa zinazoweza kuingia sokoni, ikiwemo sabuni, vinywaji na bidhaa nyingine.
Kwa upande mwingine, amesema wanaendelea kushirikiana na jamii, hususan vikundi vya wanawake na wajasiriamali wa vijijini, kwa kuwapatia elimu na ushauri wa namna ya kutumia rasilimali walizonazo kuanzisha na kukuza biashara.
Aidha, amebainisha majukumu makuu ya chuo hicho ni kufundisha, kufanya utafiti na kutoa huduma za kitaalamu kwa jamii, huku kikitenga bajeti kwa ajili ya tafiti zinazolenga kutatua changamoto za maendeleo kwenye jamii.
Profesa Mayaya ameeleza namna chuo hicho kinajivunia watafiti wake watatu, ambao ni Profesa Provident Dimoso, Dkt. Rwezaula na Dkt. Biaro, waliotambuliwa kwa kufanya utafiti bora kupitia tuzo iliyotolewa na Wizara ya elimu ya chapisho bora lenye hadhi ya juu Duniani, akisema mafanikio hayo yanaongeza hamasa kwa watafiti wengine kuendelea kuzalisha tafiti zenye manufaa kwa jamii.
Amesema chuo kitaendelea kuwekeza katika elimu, utafiti na ubunifu ili kuhakikisha maarifa yanayozalishwa chuoni yanatumika katika kutatua changamoto na kuchochea maendeleo ya wananchi, hususan katika maeneo ya vijijini.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...