Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kwa kushirikiana na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) imezindua rasmi ushirikiano wa kimkakati unaowawezesha Watanzania kununua na kuuza hisa za kampuni zilizoorodheshwa DSE kwa urahisi kupitia huduma ya benki kwa njia ya simu kupitia Programu tumizi ya NBC Kiganjani.

Ushirikiano huo unaunganisha mfumo wa DSE Hisa Kiganjani na NBC Kiganjani, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma za masoko ya mitaji kwa kuwapa wananchi fursa ya kuwekeza katika hisa moja kwa moja kupitia simu zao, bila ulazima wa kufika katika ofisi za benki au taasisi za masoko ya mitaji.

Hafla fupi ya kutambulisha ushirikiano huo imefanyika mapema leo jijini Dar es Salaam ikihusisha maofisa waandamizi wa taasisi hizo akiwemo Ofisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Bw. Peter Nalitolela, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw Theobald Sabi na Mkurugenzi wa Utafiti Sera na Mipango wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) Bw Alfred Mkombo aliemuwakilisha Afisa Mtendaji Mkuu na Mkurugenzi Mtendaji wa mamlaka hiyo CPA Nicodemus Mkama.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw Theobald Sabi alisema kupitia huduma hiyo, wateja wataweza kufanya miamala ya ununuzi na uuzaji wa hisa, kupata taarifa muhimu za soko na kufuatilia thamani ya uwekezaji wao kwa njia rahisi, salama na inayopatikana wakati wowote.

“Kwetu ni furaha kutangaza ushirikiano kati ya DSE Hisa Kiganjani na NBC Kiganjani. Ushirikiano huu unawapa wateja wetu fursa ya kununua hisa moja kwa moja kupitia akaunti zao za NBC kwa kutumia NBC Kiganjani,” amesema Sabi.

Sabi alisema hatua hiyo inalenga kuondoa baadhi ya vikwazo vilivyokuwepo katika upatikanaji wa huduma za masoko ya mitaji na kuwafanya Watanzania wengi zaidi kuwa sehemu ya uchumi wa uwekezaji.

Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Bw. Peter Nalitolela alisema huduma hiyo haijawekewa mipaka kwa wateja wa NBC pekee, akieleza kuwa hata mtu ambaye si mteja wa NBC anaweza kupakua NBC Kiganjani, kufungua akaunti kwa kutumia namba yake ya NIDA na kupata fursa ya kutumia huduma hiyo.

“Tumeruhusu mfumo wetu wa DSE Hisa Kiganjani kuunganishwa na NBC Kiganjani. Mteja akiingia NBC Kiganjani ataweza kufikia huduma ya DSE Hisa Kiganjani na kununua hisa moja kwa moja,” amesema Nalitolela.

Kwa mujibu wa Nalitolela, ujio wa huduma hiyo unalenga pia kubadili mtazamo wa wananchi kuhusu matumizi ya akaunti za benki, kutoka kuzitumia kwa ajili ya kuweka akiba pekee hadi kuzitumia kama nyenzo za kukuza utajiri kupitia uwekezaji.

“Badala ya kutumia akaunti zetu kwa kuweka akiba tu, tunapaswa kuongeza tija kwa kutumia akaunti hizo kwa ajili ya uwekezaji. Kama mwananchi anavyoweza kufanya malipo mbalimbali kupitia simu yake, sasa anaweza pia kutumia simu hiyo kuwekeza kwenye hisa za kampuni mbalimbali,” amesema.

Naye Mkurugenzi wa Utafiti, Sera na Mipango wa CMSA, Alfred Mkombo, aliyemwakilisha Afisa Mtendaji Mkuu na Mkurugenzi Mtendaji wa CMSA, CPA Nicodemus Mkama, amesema kuunganishwa kwa mifumo ya NBC na DSE ni hatua muhimu katika kuongeza ushiriki wa wananchi kwenye masoko ya mitaji na dhamana.

“Uunganishwaji wa mifumo ya NBC na DSE ni hatua inayotarajiwa kuwafikisha wananchi wengi zaidi kwenye masoko ya mitaji na dhamana kupitia mifumo ya kidijitali,” amesema Mkombo.

Amesema huduma hiyo itawawezesha wateja wa NBC kufikia soko la hisa la Dar es Salaam kupitia simu zao, wakati wowote na mahali popote, hivyo kupunguza changamoto za upatikanaji wa huduma za uwekezaji.

Kwa mujibu wa Mkombo, kwa CMSA na sekta ya masoko ya mitaji kwa ujumla, huduma hiyo ni fursa muhimu ya kupanua wigo wa ushiriki wa wananchi katika uwekezaji na kuhakikisha manufaa ya masoko ya mitaji yanafika kwa sehemu kubwa zaidi ya jamii.

Hata hivyo, ameitaka NBC kuweka mkakati maalum wa elimu na uhamasishaji kwa wananchi ili kuwawezesha kuelewa kwa kina namna ya kutumia huduma hiyo pamoja na misingi ya uwekezaji katika masoko ya mitaji.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Bw. Peter Nalitolela (kulia), na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Bw. Theobald Sabi (katikati), wakionyesha alama ya ushirikiano kati ya taasisi hizo mbili wakati wa hafla ya kutangaza ushirikiano wa kimkakati unaowawezesha Watanzania kununua na kuuza hisa za kampuni zilizoorodheshwa DSE kwa urahisi kupitia huduma ya benki kwa njia ya simu ya NBC Kiganjani. Ushirikiano huo umetangazwa leo jijini Dar es Salaam wakati wa hafla fupi iliyohusisha maofisa kutoka pande zote mbili. Anayeshuhudia ni Mkurugenzi wa Utafiti, Sera na Mipango wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Bw. Alfred Mkombo.
Mkurugenzi wa Utafiti, Sera na Mipango wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Bw. Alfred Mkombo (alishika kengere katikati) akigonga kengere kuashria uzinduzi rasmi wa ushirikiano kati ya Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) unaowawezesha Watanzania kununua na kuuza hisa za kampuni zilizoorodheshwa DSE kwa urahisi kupitia huduma ya benki kwa njia ya simu ya NBC Kiganjani. Wengini ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Bw. Peter Nalitolela (wa pili kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Bw. Theobald Sabi (wa pili kulia), Mkurugenzi wa Idara ya wateja wadogo na wakubwa wa benki hiyo Bw Elibariki Masuke (kulia) na maofisa wengine kutoka taasisi hizo.Ushirikiano huo umetangazwa leo jijini Dar es Salaam wakati wa hafla fupi iliyohusisha maofisa kutoka pande zote mbili.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...