
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
TUME ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) imejipanga kutoa fursa za ajira kwa maelfu ya vijana kupitia utekelezaji wa miradi ya uchimbaji wa visima na ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji nchini.
Mpango huo unalenga kuongeza ajira kwa vijana wenye ujuzi wa uhandisi na ufundi, sambamba na kuongeza upatikanaji wa maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya 32 ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa NIRC, Raymond Mndolwa, alisema Tume imejipanga kutekeleza miradi mikubwa ya umwagiliaji ili kuwawezesha wakulima kuzalisha kwa tija na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Alisema katika kipindi cha miaka mitatu hadi minne iliyopita, Tume imefanikiwa kusimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umwagiliaji, ikiwamo uchimbaji wa visima na ujenzi wa miundombinu, huku wakandarasi 146 wakiendelea na kazi katika maeneo mbalimbali nchini na usanifu wa miradi 634 ukiendelea.
Mndolwa alisema katika mwaka wa fedha 2026/27, Tume inatarajia kuzindua zaidi ya miradi 30 ya umwagiliaji ambayo itasaidia kuongeza maeneo yanayolimwa kwa kutumia umwagiliaji na kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.
Aidha, alisema Tume imeanza kusambaza pampu za umwagiliaji katika mikoa saba, zoezi lililoanza Mkoa wa Katavi, ambapo vifaa hivyo vitawawezesha wakulima kutumia maji kutoka kwenye mito na mabonde kwa njia inayozingatia uhifadhi wa mazingira, hususan katika kilimo cha mboga na matunda.
Alisema Serikali pia imepokea zaidi ya pampu 1,000 zinazotumia nishati ya jua, ambazo zitagawiwa kwa wakulima katika maeneo ambayo hayajanufaika moja kwa moja na miradi ya umwagiliaji kutokana na jiografia ya maeneo hayo.
Kwa mujibu wa Mndolwa, pampu hizo zitasaidia wakulima kupata maji kwa urahisi na hivyo kuongeza uzalishaji wa kilimo cha umwagiliaji katika maeneo yenye changamoto ya upatikanaji wa maji.
Kuhusu uchimbaji wa visima, alisema hadi sasa visima 415 vimechimbwa, huku kazi hiyo ikiendelea katika wilaya mbalimbali nchini.
Alisema utekelezaji wa miradi hiyo utafungua fursa kubwa za ajira kwa vijana wenye taaluma za uhandisi na ufundi, ambao wataunda vikundi vitakavyowezeshwa kusimamia, kufunga na kufanya matengenezo ya miundombinu ya visima katika halmashauri 154 nchini.
Mndolwa aliwataka vijana wenye ujuzi katika fani hizo kujitokeza kutumia fursa zitakazotokana na miradi hiyo, akisema mpango huo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuongeza ajira na kukuza ushiriki wa vijana katika sekta ya kilimo.
Alisema utekelezaji wa miradi hiyo pia unalenga kuchangia kufikiwa kwa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hasa katika kuongeza mchango wa sekta ya kilimo kwenye uchumi na kuimarisha usalama wa chakula nchini.
Aliongeza kuwa Tume imeweka mpango wa kuchimba jumla ya visima 67,000 ifikapo mwaka 2035, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa maji kwa ajili ya umwagiliaji na kuwezesha maeneo mengi zaidi nchini kufanya kilimo chenye tija.




Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...