Na  Avila Kakingo
SERIKALI imewataka wamiliki na waendeshaji wa miundombinu muhimu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kukamilisha usajili wake ndani ya miezi sita, huku ikisisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuilinda dhidi ya mashambulizi ya mtandao, hitilafu na majanga.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, amesema usajili huo unalenga kuiwezesha Serikali kutambua miundombinu yenye umuhimu mkubwa kwa usalama, uchumi na ustawi wa jamii na kuhakikisha inalindwa dhidi ya vitisho vinavyoweza kuvuruga huduma muhimu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano, Agosti 19, 2026, jijini Dar es Salaam, Kairuki amesema wamiliki na waendeshaji wanatakiwa kukamilisha usajili huo ifikapo Desemba 19, 2026.

Amesema miundombinu muhimu ya TEHAMA inahusisha mali, vifaa, mifumo ya kompyuta na mitandao inayoshikika na isiyoshikika ambayo endapo itashindwa kufanya kazi inaweza kusababisha madhara makubwa kwa usalama, uchumi na jamii.

Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha miundombinu hiyo inaendelea kuwa salama, inapatikana na kufanya kazi kwa uhakika hata wakati wa mashambulizi ya mtandao, hitilafu za kiufundi au majanga.

Kwa mujibu wa Kairuki, sekta zenye miundombinu hiyo ni pamoja na habari na mawasiliano, fedha na benki, maji, afya, nishati, madini, usafirishaji, chakula na kilimo, ujenzi, uchumi wa buluu, mazingira, viwanda, ulinzi, anga, elimu, utawala wa kiraia, ulinzi wa raia, ardhi pamoja na usalama na utulivu wa umma.

Amesema hatua hiyo inatekelezwa kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Mtandao Namba 14 ya mwaka 2015, hususan Kifungu cha 28(1), kinachompa Waziri mwenye dhamana ya mawasiliano mamlaka ya kutangaza miundombinu muhimu ya TEHAMA.

“Ni lazima kwanza itambuliwe kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa kisheria. Ulinzi wa miundombinu hiyo unalenga kuhakikisha inabaki salama, inapatikana na inafanya kazi kwa uhakika hata wakati kunapotokea mashambulizi ya mtandao, hitilafu au majanga,” amesema.

Kairuki amesema uharibifu wa miundombinu hiyo unaweza kusababisha madhara makubwa ya kiusalama na kiuchumi na kwamba sheria imeweka adhabu kwa mtu atakayebainika kufanya uharibifu huo.

Amesema kwa mujibu wa Kifungu cha 29 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, mhusika anaweza kutozwa faini isiyopungua Sh100 milioni au mara tatu ya hasara iliyosababishwa, kifungo kisichopungua miaka mitano au adhabu zote kwa pamoja.

Amesema Serikali imeandaa miongozo mitano itakayowawezesha wamiliki na waendeshaji wa miundombinu muhimu ya TEHAMA kuelewa wajibu wao katika kuitambua, kuisimamia na kuilinda.

Miongozo hiyo inahusu utambuzi na usimamizi wa miundombinu muhimu ya TEHAMA, ukaguzi, tathmini ya hatari, uadilifu na uhalisia wa data pamoja na mipango ya urejeshaji wa huduma baada ya janga.

Amesema wamiliki na waendeshaji wa miundombinu hiyo wanapaswa kutumia mfumo maalumu wa CII Portal kwa ajili ya usajili na kuwasilisha taarifa zinazohitajika kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.

Aidha, Kairuki amesema changamoto za kiusalama zinazohusisha miundombinu muhimu ya TEHAMA zinapaswa kuripotiwa kwa mamlaka husika ndani ya saa 24 tangu kubainika kwake.

Akizungumza na Mwananchi, Mkurugenzi wa Mawasiliano, Munaku Mulemwa, amesema usajili huo ni hatua muhimu katika kujenga mazingira salama na imara ya kidijitali yatakayowezesha huduma muhimu kuendelea kutolewa kwa ufanisi licha ya kuongezeka kwa vitisho vya usalama wa mtandao.

Amesema usajili utaiwezesha Serikali kuwa na uelewa wa miundombinu inayohitaji ulinzi maalumu, kutathmini vihatarishi vinavyoweza kuiathiri na kuweka mazingira bora ya kuilinda dhidi ya vitisho vinavyoendelea kuongezeka.

“Hatua hii inasaidia sana kutambua miundombinu hiyo, kutathmini vihatarishi vinavyoweza kuiathiri na kuweka mazingira bora ya kuilinda dhidi ya vitisho vinavyoendelea kuongezeka katika ulimwengu wa sasa,” amesema Mulemwa.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...