Na George Maziku, Mbogwe
WACHIMBAJI wadogo katika mgodi wa dhahabu wa Mwinula Group Gold Rush uliopo kijiji cha Mgaya, kata ya Lugunga, wilayani Mbogwe, mkoa wa Geita wamemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuwasaidia kupata umeme katika mgodi wao ili kuwarahisishia kazi ya uchimbaji na uchenjuaji dhahabu.
Wachimbaji hao wametoa kilio chao mbele ya waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari waliotembelea mgodi huo Jumatatu, Agosti 10, mwaka huu.
Akizungumzia adha wanayopata kutokana na ukosefu wa umeme mgodini hapo, katibu mkuu wa mgodi huo Jesto Shashu alisema wamekuwa wakitumia gharama kubwa katika uchimbaji na uchenjuaji kutokakana na matumizi ya nishati ya mafuta ambayo kwa sasa yamepanda bei, hali inayowasababishia hasara kubwa.
“Hali ya kukosa umeme pia imesababisha mgodi wetu kukikmbiwa na wawekezaji, kama ambavyo mnaona wenyewe ndugu waandishi idadi ya duara zinazofanya kazi ni ndogo sana baada ya wawekezaji wengine kutelekeza duara zao na kuondoka kutokana na kulemewa na gharama za uchimbaji”, alibainisha Shashu.
Mgodi huo ulioanza miaka mitatu iliyopita kwa sasa umeshuka katika uzalishaji, hali ambayo imewalazimisha watu wengi wanaonufaika na uchimbaji, wakiwemo wachimbaji, wabeba mizigo ya mawe, bodaboda, mamalishe, wafanyabiashara mbalimbali, kukimbilia migodi mingine ambayo uzalishaji upo juu.
Katibu huyo amesema kuwa mgodi wake una uwezo mkubwa wa kuzalisha ikiwa utapatiwa umeme, na kuzidi kumlilia Rais Samia kuwaelekeza wasaidizi wake kupeleka umeme kwa haraka katika mgodi huo.
“Mwamba wa dhahabu uliopo kwenye mgodi wetu ni mkali sana, na kama serikali ya mama yetu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ikitupatia umeme mwaka huu, tunaweza kuwa mgodi mkubwa sana ndani ya muda mfupi na kuwavutia watu wengi”, alifafanua Shashu.
Aliongeza kuwa, “Tunamuomba sana Rais wetu atusaidie kutuletea umeme tuweze kuzalisha mawe ya kutosha ili serikali yenyewe ipate mapato makubwa na sisi wachimbaji na watu wengine wanaotegemea mgodi wetu tunufaike”, alisisitiza katibu huyo.




.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...