Na Belinda Joseph, Dodoma

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo, amesema matumizi ya taarifa sahihi za masoko ni nyenzo muhimu katika kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania, kukuza mauzo ya nje na kuvutia uwekezaji wa kimkakati unaochochea ukuaji wa uchumi.

Mhe. Londo ameyasema hayo Agosti 7, 2026, katika Viwanja vya Nane Nane, jijini Dodoma, wakati akifungua mkutano wa Intelijensia ya Masoko na Matokeo, ulioandaliwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), uliowakutanisha wadau mbalimbali kujadili namna taarifa za masoko zinavyoweza kutumika kuchochea biashara na maendeleo ya viwanda.

Amesema mabadiliko ya teknolojia, mahitaji ya walaji na mifumo ya uzalishaji na usambazaji yanaendelea kufungua fursa mpya za biashara, hivyo Tanzania inapaswa kuendelea kutumia taarifa za masoko kuwawezesha wazalishaji na wafanyabiashara kufanya maamuzi sahihi na kuongeza ushindani katika masoko ya kikanda na kimataifa.

“Tunapaswa kuzalisha kwa kuzingatia mahitaji ya soko na kutumia taarifa sahihi za masoko katika kufanya maamuzi ya uzalishaji, uwekezaji na biashara,” amesema.

Ameeleza kuwa juhudi za Tanzania kujenga uchumi wa kisasa unaotegemea viwanda na kuongeza mauzo ya bidhaa nje ya nchi zinahitaji ushirikiano madhubuti kati ya Serikali, sekta binafsi na taasisi mbalimbali, ili kuhakikisha wazalishaji na wafanyabiashara wanapata taarifa muhimu za masoko kwa wakati.

Aidha, amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa biashara na uwekezaji, pamoja na kuhamasisha uzalishaji wa bidhaa zenye ubora na viwango vinavyokidhi mahitaji ya masoko ya kimataifa, hatua itakayosaidia kuongeza thamani ya bidhaa na fursa za mauzo nje ya nchi.

Mhe. Londo amesema matumizi ya taarifa sahihi za masoko yatawawezesha wazalishaji kubaini mahitaji na fursa zilizopo katika masoko mbalimbali, kupanga uzalishaji kulingana na mahitaji ya walaji na kuimarisha uwezo wa bidhaa za Tanzania kushindana katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Amesisitiza kuwa mafanikio ya juhudi hizo yanahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na sekta binafsi, huku akieleza kuwa kuunganisha taarifa za masoko na uzalishaji, uongezaji thamani na biashara kutasaidia kuongeza kipato cha wananchi, kutengeneza ajira na kuchochea ukuaji jumuishi wa uchumi.

Akihitimisha hotuba yake, Mhe. Londo amesema matumizi madhubuti ya taarifa za masoko, sambamba na uwekezaji katika uzalishaji na uongezaji thamani, ni msingi muhimu katika kujenga uchumi imara na wenye ushindani, huku Tanzania ikiendelea kutumia fursa zinazotokana na masoko ya kikanda na kimataifa.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...