Na Janeth Raphael - MichuziTv 

Serikali imewataka wanawake nchini kuwa waangalifu wanapochukua mikopo, ikisisitiza waepuke mikopo yenye masharti yanayoweza kusababisha migogoro ya kifamilia, kuvunjika kwa ndoa au kupoteza mali zao. Badala yake, imewahimiza kutumia elimu wanayopewa kuchagua mikopo yenye tija itakayowasaidia kukuza biashara na kujikwamua kiuchumi.

Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Amon Mpanju, wakati akifungua Jukwaa la Tatu la Wanawake wa Ushirika Taifa 2026, lililowakutanisha wanawake kutoka vyama mbalimbali vya ushirika kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kiuchumi na uongozi.

Katika hafla hiyo, Dkt. Mpanju pia alizindua Mwongozo wa Jukwaa la Wanawake wa Ushirika Taifa, akieleza kuwa utakuwa nyenzo muhimu ya kuwaongoza wanawake katika uendeshaji wa shughuli zao za ushirika, kuimarisha ushiriki wao katika maamuzi na kuongeza mchango wao katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za ushirika na wadau mbalimbali kuhakikisha wanawake wanapata mazingira bora ya kushiriki katika shughuli za uzalishaji, ujasiriamali na maendeleo, huku akisisitiza kuwa uwezeshaji wa wanawake ni msingi wa kujenga uchumi imara wa taifa.

Akizungumza katika jukwaa hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC), Farres Muganda, amewataka wanawake wanaoshiriki katika vyama vya ushirika kuongeza uelewa kuhusu masoko, matumizi ya teknolojia na usimamizi wa shughuli za kiuchumi ili kuongeza tija na ushindani.

Muganda amesema wanawake wanahitaji kupata taarifa sahihi kuhusu fursa za masoko na kuendelea kujifunza ili waweze kutumia ipasavyo teknolojia katika uzalishaji na biashara zao. Alieleza kuwa TFC itaendelea kuimarisha jukwaa hilo ili liwe kitovu cha kuwajengea wanawake uwezo wa kushiriki kikamilifu katika maendeleo kupitia mfumo wa ushirika.

Ameongeza kuwa wanawake pamoja na vijana wanapaswa kupewa nafasi zaidi katika shughuli za ushirika kwani makundi hayo yana mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa familia na taifa kwa ujumla.

Aidha, Muganda amesema pamoja na uwepo wa majukwaa zaidi ya 15,000 ya wanawake nchini, bado changamoto ya upatikanaji wa mitaji na mikopo yenye masharti nafuu inaendelea kuathiri ukuaji wa shughuli zao za kiuchumi.

Amewataka wanawake kutumia elimu wanayoipata kupitia majukwaa hayo kufanya maamuzi sahihi ya kifedha, kusimamia shughuli zao kwa ufanisi, kuzingatia sheria na kanuni za ushirika na kutumia fursa za masoko pamoja na teknolojia ili kujenga ushirika wenye tija na kuboresha maisha yao.








Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...