Wananchi wenye amana katika benki iliyowekwa chini ya ufilisi ya FBME wamehimizwa kujitokeza kuchukua fedha zao baada ya kubainika kuwa zaidi ya Sh bilioni 2.9 za fidia zinazolindwa na Bima ya Amana bado hazijachukuliwa na wamiliki wake. 

Wito huo umetolewa na Meneja wa Fedha na Uhasibu wa Bodi ya Bima ya Amana (DIB), Romuli Mtui, alipozungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya Nanenane Kitaifa yanayoendelea jijini Dodoma Agosti 6, 2026.

Mtui amesema wateja ambao hawajachukua fidia ya kiwango kinacholindwa na Bima ya Amana wanapaswa kufika katika matawi ya Benki ya Biashara ya TCB ili kulipwa, huku wale waliolipwa sehemu ya fedha zao lakini bado wanadai salio la amana zao wakiendelea kufuatilia madai yao katika ofisi za Bodi ya Bima ya Amana zilizopo ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) jijini Dar es Salaam na Dodoma. 

Aidha, amesema malipo ya fidia kwa wateja waliokuwa na amana katika Benki ya FBME upande wa Tanzania tayari yameanza, hivyo wameelekezwa kufuatilia madai yao kupitia ofisi za bodi hiyo au mawasiliano yaliyotolewa kwenye tovuti yake.

Ameongeza kuwa tangu mwaka 2000 jumla ya benki tisa zimewekwa chini ya ufilisi nchini, huku benki saba zilizowekwa chini ya ufilisi mwaka 2017 na 2018 zikiendelea na zoezi la ufilisi ambazo ni  Benki ya Wananchi Mbinga, Benki ya Wananchi Njombe, Benki ya Wakulima Kagera, EFATA Community Bank na FBME Bank, akisisitiza kuwa wateja wote ambao bado hawajachukua fedha zao wanapaswa kujitokeza ili walipwe stahiki zao.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa DIB, Lwaga Mwambande, amesema kila mteja anayefungua akaunti katika benki yenye leseni ya BoT hunufaika na kinga ya amana bila kuchangia moja kwa moja, kwa kuwa michango ya Mfuko wa Bima ya Amana hulipwa na benki wanachama. 

Amesema kiwango cha juu cha fidia kinacholipwa kwa sasa ni Sh milioni 7.5 kwa kila mwekaji endapo benki itafutiwa leseni na kushindwa kuendelea na shughuli zake.

Mwambande amefafanua kuwa wateja wenye amana zinazozidi kiwango hicho hawapotezi fedha zao moja kwa moja, kwani baada ya benki kufungwa huanza mchakato wa ufilisi ambapo mali za benki hukusanywa na kugawiwa kwa wadai kwa mujibu wa sheria, benki zote zinazopokea amana kutoka kwa wananchi huchangia asilimia 0.15 ya amana zao kwa mwaka katika Mfuko wa Bima ya Amana ili kuimarisha uwezo wa kulipa fidia kwa waweka amana.

Amesema pamoja na jukumu la kulipa fidia na kuendesha ufilisi wa benki zilizofungwa, Bodi ya Bima ya Amana pia ina wajibu wa kupunguza hasara kwa kusaidia benki zinazokumbwa na changamoto za kifedha kabla hazijafungwa kupitia utoaji wa mtaji, dhamana au mikopo, hatua inayolenga kuimarisha uthabiti wa sekta ya fedha nchini.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...