*Nicolaus Mboya ndio Afisa Mtendaji Mkuu wa Sparks 360 Hub

Na Mwandishi Wetu, Tanga
MHITIMU wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Nicolaus Mboya Mwakampya, amesema mpango wa taasisi hiyo wa kukuza na kuendeleza vipaji na ubunifu umemwezesha kujiajiri na kutoa ajira kwa vijana wengine.

Mboya ni miongoni mwa wahitimu wa TIA walionufaika na mpango huo, ambapo ameibua ubunifu wa kiteknolojia unaolenga kuwafundisha watoto matumizi ya teknolojia mbalimbali tangu wakiwa katika ngazi za awali za elimu.

Akizungumza katika Maonesho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yanayoendelea katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara jijini Tanga, Mboya alisema teknolojia hiyo inalenga kuwajengea watoto uelewa wa teknolojia mapema na hivyo kuongeza idadi ya wataalamu wa teknolojia nchini.

Alisema ubunifu wake unahusisha maeneo mbalimbali ikiwemo Robotics, 3D Printing, Electronic Coding, Akili Unde (AI) pamoja na sanaa ya uchoraji.

Mboya alisema baada ya kuhitimu TIA, aliendeleza wazo alilolianzisha chuoni na baadaye kuanzisha kampuni inayojulikana kama Sparks 360 Hub, ambayo kwa sasa imeweza kutoa ajira kwa vijana wengine wanane, yeye akiwa Afisa Mtendaji Mkuu.

“Mpango wa TIA wa kukuza na kuendeleza vipaji na taaluma umenisaidia sana kuendeleza wazo langu, ambalo sasa limekuwa kampuni na kutoa fursa za ajira kwa vijana wengine,” alisema Mboya.

Alisema hadi sasa kampuni hiyo imewafikia zaidi ya watu 500 pamoja na shule sita, huku ikiendelea kuweka mikakati ya kupanua huduma na kusambaza teknolojia hiyo ya kufundishia watoto katika maeneo mbalimbali nchini.

Mboya alisema TIA imeendelea kutoa mwongozo na usimamizi katika kuboresha ubunifu huo, hatua ambayo imewezesha wazo hilo kuwa suluhisho la changamoto za kiteknolojia miongoni mwa watoto.

Aidha, alisema mpango wa TIA wa kuendeleza mawazo na ubunifu wa wanafunzi una nafasi kubwa katika kuongeza fursa za ajira, hususan kwa vijana wanaohitimu katika vyuo mbalimbali.

“Ubunifu unaotokana na wanafunzi unaweza kuwa chanzo cha kujiajiri na pia kutoa suluhisho la changamoto mbalimbali zinazolikabili Taifa. Ni muhimu kutumia maarifa tunayopata vyuoni kubuni teknolojia zitakazokuwa na manufaa kwa jamii,” alisema.
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...