Na Mwandishi Wetu, Tanga
MWANAFUNZI wa mwaka wa tatu wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Brayan Kachocho, amebuni mfumo wa kidijitali unaojulikana kama Biashara Yangu, unaowawezesha wafanyabiashara kusimamia shughuli zao za biashara kwa urahisi wakiwa mahali popote.
Kachocho, anayesoma Sayansi ya Kompyuta, alisema mfumo huo unamwezesha mfanyabiashara kupata taarifa muhimu za biashara ikiwemo mauzo, manunuzi, bidhaa zilizopo stoo pamoja na taarifa nyingine kupitia simu au kompyuta.
Akizungumza katika Maonesho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yanayoendelea katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara jijini Tanga, Kachocho alisema mfumo huo unalenga kuwasaidia wafanyabiashara kupata taarifa za biashara zao kwa wakati na kufanya maamuzi kwa haraka.
Alisema teknolojia hiyo inaweza kusaidia wafanyabiashara kupunguza changamoto za upotevu wa taarifa, kuongeza ufanisi na kuboresha usimamizi wa biashara zao.
Kachocho alisema amekuwa miongoni mwa wanafunzi walionufaika na mpango wa IFM wa kukuza na kuendeleza vipaji na taaluma, jambo lililomsaidia kuboresha wazo lake na hatimaye kuanzisha kampuni.
“Nimekuwa miongoni mwa wanafunzi wanaonufaika na mpango wa IFM wa kukuza na kuendeleza vipaji na taaluma, jambo linalonisaidia kuendeleza wazo ambalo sasa tumeanzisha kampuni,” alisema.
Alisema kupitia ubunifu huo amesajili kampuni ya Afrinova, ambayo hadi sasa imefikia watumiaji 50, huku huduma ya mfumo huo ikitolewa kwa gharama ya Sh5,000 kwa mwezi kwa mfanyabiashara.
Aidha, Kachocho alisema IFM imekuwa ikitoa mwongozo na usimamizi katika kuboresha mawazo na ubunifu wa wanafunzi, hatua inayowasaidia kubadilisha maarifa wanayopata darasani kuwa suluhisho la changamoto za jamii.
Alitoa wito kwa vijana kutumia maarifa wanayopata vyuoni kubuni teknolojia na bidhaa zitakazokuwa na manufaa kwa jamii badala ya kutegemea ajira baada ya kumaliza masomo.
“Ubunifu unaotokana na wanafunzi unaweza kuwa chanzo cha kujiajiri na pia kutoa suluhisho la changamoto mbalimbali zinazolikabili Taifa,” alisema.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...