NA: MWANDISHI WETU, PANGANI
Viongozi na watendaji wa matawi wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), wilaya ya Pangani mkoani Tanga, wamepatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa masuala mbalimbali ya kichama, kiuongozi na kijamii ili kuboresha utendajikazi wao wa kila siku.
Mafunzo hayo yametolewa Agosti 2, 2026, katika Kata ya Kipumbwi wilayani humo.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Mwenyekiti wa Seneti ya vyuo vya kati, vyuo na vyuo vikuu mkoa wa Tanga, Leila Mnaki, ambaye alikuwa miongozo mwa wakufunzi, amesema CCM ni Chama imara kwani misingi yake ipo ngazi za chini za mabalozi na matawi, hivyo ni wajibu wa Chama kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa viongozi wake ili kuboresha utendajikazi.
"Nguvu ya Chama ni wanachama na viongozi wake, ndiyo maana tupo hapa kupata mafunzo ya kutujengea uwezo ili utendajikazi wetu uwe wenye tija kwa manufaa ya Chama na wananchi tunaowahudumia," amesema Mnaki.
Aidha, Mnaki amesema, ni wajibu wa viongozi kuwahudumia wananchi kwa kufuata misingi ya Chama, ambayo imesisitiza kutanguliza maslahi ya wananchi ili kukuza maendeleo.
"Chama chetu hakiongozwi kwa utashi wa mtu, bali kanuni, miongozo na taratibu, ni matumaini yangu kuwa viongozi na watendaji mtazingatia hili katika Utumishi wenu wote," ameongeza.
Awali, mratibu wa mafunzo hayo, ambaye pia ni Katibu wa UVCCM wilaya, Nasri Mkalipa, aliwasisitiza viongozi hao kuzingatia yote na kuyatendea kazi.
"Niwasihi sana tuzingatie yote tutakayofundishwa hapa, kwani mafunzo haya ni mahsusi katika kuboresha utendajikazi wetu na kuonyesha utofauti wa kiuongozi," amesema Mkalipa.
Katika mafunzo hayo, mada mbalimbali zilifundishwa kwa viongozi hao. Miongoni mwa mada hizo ni pamoja na itikadi, kanuni na falsafa ya CCM, uandishi wa muhtasari na utunzaji kumbukumbu.
Pia, masuala ya uongozi wa kimkakati, ukatili wa kijinsia, afya ya akili, usalama barabarani na matumizi ya mitandao ya kijamii.
Ikumbukwe kuwa, mafunzo hayo maalum yamepewa jina la "Darasa la Ushindi" huku yakichagizwa na kaulimbiu ya "T3 - Tujifunze, Tuongoze na Tuwajibike".
Kimsingi, mkakati uliopo ni kufikisha mafunzo hayo katika kata zote 14 za wilaya hiyo, huku walengwa wa mafunzo hayo wakiwa ni wenyeviti, makatibu na makatibu hamasa wa UVCCM wa matawi yote wilayani humo.



.jpeg)



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...