Kampuni ya mawasiliano ya Yas Tanzania imezindua rasmi mnara wa 5G wilayani Masasi, Mkoa wa Mtwara, hatua inayotarajiwa kuongeza kasi ya biashara, kuboresha upatikanaji wa huduma za kidijitali na kufungua fursa mpya za maendeleo kwa wakazi wa wilaya hiyo na maeneo ya jirani.

Uwekezaji huo ni sehemu ya mkakati wa Yas wa kuendelea kusogeza teknolojia ya kisasa karibu na wananchi ili kuwawezesha kunufaika na uchumi wa kidijitali kupitia mawasiliano yenye kasi, uhakika na ubora.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Yas Kanda ya Pwani Kusini, Bi. Fadhila Saidi, alisema kampuni inaendelea kuwekeza katika miundombinu ya kisasa ya mawasiliano ili kuhakikisha Watanzania wanapata suluhisho zinazowawezesha kuboresha maisha na kukuza shughuli zao za kiuchumi.

"Tunazindua mnara huu wa 5G kwa lengo la kuhakikisha wakazi wa Masasi na mkoa wa Mtwara kwa ujumla wanapata huduma za mawasiliano zenye kasi na ubora ili kuchochea shughuli za kiuchumi na mawasiliano ya uhakika. Kwetu sisi, teknolojia ni nyenzo ya kuwawezesha Watanzania kufikia fursa zaidi za maendeleo," alisema Bi. Saidi.

Aliongeza kuwa, Wilaya ya Masasi ina wakazi zaidi ya 315,000 wanategemea kilimo na biashara, hivyo uzinduzi wa teknolojia ya 5G wilayani humo utachochea shughuli mbalimbali za kimaendeleo, kwani wakulima wataweza kufuatilia bei za mazao na kuwasiliana moja kwa moja na masoko, huku wafanyabiashara wakipanua biashara zao kupitia majukwaa ya kidijitali na mifumo ya kisasa ya malipo”.

Bi. Saidi alisema huduma hiyo pia itawanufaisha vijana kwa kuwafungulia fursa za ajira, ubunifu na ujasiriamali kidijitali, huku wanafunzi na walimu wakipata urahisi wa kutumia majukwaa ya kujifunzia mtandaoni. Aidha, taasisi za afya na huduma nyingine za kijamii zitanufaika na mawasiliano yenye kasi na uhakika yatakayoongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.

Aliongeza kuwa, sambamba na uwekezaji katika mawasiliano, kwa upande wa Mixx, Kampuni inaendelea kuwawezesha wananchi kutuma na kupokea fedha, kulipa bili, kufanya malipo ya biashara na kupata huduma mbalimbali za kifedha kwa usalama na urahisi, hatua inayochochea ujumuishaji wa kifedha na ukuaji wa uchumi wa wananchi.

Kwa upande wake, mkazi wa Masasi na mfanyabiashara, Bw. Jaffari Wadi, alisema uzinduzi wa mnara huo wa 5G utakuwa chachu ya kukuza biashara katika eneo hilo.

"Uzinduzi wa mnara huu wa 5G utatusaidia kwa kiasi kikubwa kuchochea ukuaji wa biashara zetu kwani huduma sasa zitakuwa za haraka zaidi. Tutakuwa na uwezo wa kuwasiliana kwa urahisi na wateja, kufanya miamala kwa wakati na kutumia fursa za biashara mtandaoni ambazo hapo awali zilikuwa changamoto kutokana na kasi ya mtandao," alisema Bw. Wadi.

Yas imeendelea kuwekeza katika upanuzi wa mtandao wake nchini ikiwa ni sehemu ya dhamira yake ya kuhakikisha hakuna Mtanzania anayebaki nyuma katika safari ya mageuzi ya kidijitali. Kampuni hiyo inaamini kuwa upatikanaji wa miundombinu ya mawasiliano yenye ubora ni msingi wa kukuza biashara, kuimarisha ujumuishaji wa kidijitali na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Uzinduzi wa mnara wa 5G Masasi unaongeza hatua nyingine katika juhudi za Yas za kuendelea kuwapatia Watanzania suluhisho za mawasiliano na kifedha zinazowawezesha kufungua fursa mpya za maendeleo na kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali.
Mkuu wa Yas Kanda ya Kusini, Bi. Fadhila Saidi (kulia), akiwa pamoja na Mwenyekiti wa Mtaa wa Majimaji, Wilaya ya Masasi, Bw. Bakari Issa (kushoto), wakikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa mnara wa 5G wa Yas katika Wilaya ya Masasi, Mkoa wa Mtwara, hivi karibuni. Teknolojia hiyo inatarajiwa kuboresha huduma za intaneti ya kasi, kuchochea ukuaji wa biashara na kuongeza upatikanaji wa huduma za kidijitali kwa wakazi wa Masasi na maeneo ya jirani.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...