Na Janeth Raphael – MichuziTv - Bungeni Dodoma
SERIKALI imesema maandalizi ya Tanzania kuwa mwenyeji wa Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 yanaendelea kwa kasi, huku ikihakikisha miundombinu muhimu ya michezo na huduma wezeshi inakamilishwa kwa wakati.
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema hayo leo, Ijumaa, Septemba 4, 2026, jijini Dodoma, wakati akiwasilisha hoja ya kuahirisha Bunge la 13, Mkutano wa Nne.
Amesema kazi zinazoendelea zinahusisha ujenzi na ukarabati wa viwanja vya mashindano na mazoezi, barabara zinazounganisha maeneo ya viwanja, pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa huduma muhimu za afya, maji na umeme.
Kwa upande wa viwanja, Dkt. Mwigulu amesema ujenzi wa Uwanja wa Jiji la Arusha umefikia zaidi ya asilimia 91, huku ujenzi wa uwanja mwingine wenye uwezo wa kuchukua zaidi ya watazamaji 32,000 ukiendelea.
Amesema kwa upande wa Dar es Salaam, ukarabati wa Uwanja wa Benjamin Mkapa pamoja na viwanja vya mazoezi umekamilika, hatua inayoongeza utayari wa jiji hilo katika maandalizi ya mashindano hayo.
Kwa upande wa Zanzibar, Serikali imeeleza kuwa Uwanja wa Fumba unaendelea katika hali nzuri, huku miundombinu mingine ikiwemo New Amaan Complex, Amaan Annex One na Annex Two ikiwa imekamilika. Aidha, Uwanja wa Amaan umeelezwa kuwa katika hali nzuri kwa matumizi ya mashindano.
Dkt. Mwigulu amewataka wasimamizi wa miradi kuhakikisha fedha zinazowekezwa katika maandalizi ya AFCON 2027 zinazalisha thamani inayolingana na uwekezaji huo, akisisitiza kuwa Tanzania inapaswa kutumia nafasi ya kuwa mwenyeji wa mashindano hayo kupata manufaa ya kiuchumi.
Amesema wizara na taasisi zinazohusika zinapaswa kuendelea kuratibu mikakati itakayowezesha Tanzania kunufaika kikamilifu na fursa zitakazotokana na uenyeji wa mashindano hayo, huku akiwataka wadau wote kushiriki kikamilifu ili kuepusha vikwazo vinavyoweza kupunguza ufanisi na manufaa yanayotarajiwa.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesisitiza umuhimu wa Tanzania kuwa na timu ya taifa yenye ushindani wakati wa mashindano hayo, akisema mwenyeji hapaswi kuwa mshiriki wa kawaida au “msindikizaji”.
“Sisi ni wenyeji wa mashindano, hivyo tunapenda kuona timu ya taifa pia inakuwa na ubora na sio msindikizaji,” amesema Dkt. Mwigulu.
Amewataka makocha, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na benchi la ufundi kuanza mapema kuweka mikakati maalumu itakayoiwezesha timu ya taifa kufanya vizuri katika AFCON 2027.
Tanzania itakuwa miongoni mwa wenyeji wa AFCON 2027 pamoja na Kenya na Uganda, hali inayoiweka nchi katika nafasi ya kutumia mashindano hayo kukuza sekta ya michezo, utalii, biashara na shughuli nyingine za kiuchumi.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...