Na Karama Kenyunko Michuzi tv
SERIKALI imebadilisha ratiba ya Upimaji na Mitihani ya Taifa ya mwaka 2026, kwa kurudisha nyuma mitihani hiyo kutoka Novemba hadi Oktoba, kutokana na utabiri wa mvua kubwa za El Niño unaotarajiwa kuathiri maeneo mbalimbali nchini.
Hatua hiyo imetangazwa leo Septemba 25, 2026, huku Serikali ikieleza kuwa hatua hiyo imelenga kulinda usalama wa wanafunzi, walimu, wasimamizi na maofisa wengine, pamoja na mitihani, vifaa na nyaraka zake.
Akizungumza na waandishi wa Habari, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Amneir, amesema Serikali imechukua hatua hiyo baada ya kuzingatia uwezekano wa mvua kubwa kunyesha mwezi Novemba 2026, kipindi ambacho baadhi ya mitihani ilikuwa imepangwa kufanyika.
Amesema kwa mujibu wa utabiri wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) wa Agosti 18, 2026, kuna uwezekano wa kutokea kwa El Niño yenye nguvu, inayotarajiwa kuathiri mvua za Vuli kuanzia Oktoba hadi Desemba 2026 na kuendelea hadi Januari 2027.
“Kwa mujibu wa utabiri huo, mvua hizo zinatarajiwa kuanza mwezi Oktoba 2026, huku mwezi Novemba 2026 ukitarajiwa kuwa na mvua nyingi zaidi,” amesema
Amesema Serikali, kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), imeona umuhimu wa kufanya marekebisho ya ratiba ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua hizo.
Wanu amesema mvua kubwa zinaweza kusababisha mafuriko, kuathiri barabara na usafiri, hali ambayo inaweza kuchelewesha au kuzuia ufikishaji wa mitihani, vifaa na nyaraka katika vituo vya mitihani.
Amesema pia mvua hizo zinaweza kusababisha wanafunzi, wasimamizi na maofisa wengine kushindwa kufika vituoni kwa wakati, huku kukatika kwa umeme na kuathirika kwa mawasiliano kukiwa ni changamoto nyingine inayoweza kujitokeza.
Aidha, amesema mvua na unyevunyevu vinaweza kuathiri mazingira ya afya na usafi katika baadhi ya vituo vya mitihani, hususan maeneo yenye changamoto katika mifumo ya maji, vyoo na taka.
Amesema Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Pili unahusisha shule 21,353, huku wa Darasa la Nne ukihusisha shule 21,008, hivyo athari za mvua katika vituo vya upimaji zinaweza kuwakabili wanafunzi wengi.
Amesema wanafunzi wanaofanya upimaji huo wengi wao wana umri wa chini ya miaka 11, hivyo wanahitaji mazingira salama na rafiki wakati wa kufika na kushiriki katika upimaji.
Wanu ametoa wito kwa Kamati za Mitihani za Mikoa na Halmashauri pamoja na Wakuu wa Shule kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na NECTA katika kutekeleza maelekezo yatakayotolewa.
Pia amewataka wanafunzi, wazazi na walezi kuendelea kufuatilia taarifa rasmi zitakazotolewa na Wizara na NECTA kuhusu ratiba na maelekezo ya uendeshaji wa Upimaji na Mitihani ya Taifa kwa mwaka 2026.
Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa NECTA, Profesa Said Mohamed, Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne ambao awali ulipangwa kufanyika Oktoba 21 na 22, sasa utafanyika Oktoba 5 na 6, 2026.
Amesema Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Pili uliokuwa ufanyike Novemba 17 na 18, sasa utafanyika Oktoba 7 na 8, 2026.
Aidha, Upimaji wa Kitaifa wa Kidato cha Pili uliopangwa kufanyika Novemba 2 hadi 13, sasa utafanyika Oktoba 12 hadi 23, 2026.
Kwa upande wa Mtihani wa Kidato cha Nne, ambao awali ulipangwa kuanza Novemba 9 hadi 27, sasa utaanza Oktoba 19 na kukamilika Novemba 6, 2026.
Profesa Said amesema marekebisho hayo yanalenga kuhakikisha kalenda ya mitihani na mihula katika sekta ya elimu haiathiriki, huku wanafunzi wakifanya mitihani katika mazingira salama.
“Uamuzi huu umezingatia zaidi usalama wa watoto, usalama wa mitihani na kuunga mkono juhudi za Serikali kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño, hasa mwezi Novemba ambao unatabiriwa kuwa na mvua nyingi zaidi,” amesema.



.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...