Na Karama Kenyunko Michuzi tv
TANZANIA inatarajia kutumia Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi (COP12), unaofanyika Dar es Salaam Septemba 6 hadi 9, 2026, kuimarisha diplomasia ya mazingira na kuvutia fedha, teknolojia na uwekezaji katika Uchumi wa Buluu.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, amesema Tanzania imepata fursa hiyo ikiwa mwenyeji wa mkutano huo, unaotarajiwa kuongeza ushawishi wa nchi katika masuala ya mazingira ya bahari na pwani katika ngazi ya kikanda na kimataifa.

Amesema COP12 inatarajiwa kujadili na kupitisha maamuzi ya Mkutano wa Nchi Wanachama pamoja na Joint Ministerial Declaration, huku pia ikifanya uchaguzi wa Baraza la Viongozi kwa kipindi cha 2026/2028.

Kwa mujibu wa Masauni, mkutano huo unatarajiwa kutoa Azimio la DSM litakalolenga kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika Uchumi wa Buluu, ikiwemo kuongeza fursa za uvuvi endelevu, ufugaji viumbe maji, utalii wa baharini, usafiri wa majini na uwekezaji unaozingatia mazingira.

Amesema Tanzania pia inatarajia kutumia mkutano huo kuvutia fedha, teknolojia na uwekezaji kwa ajili ya uhifadhi wa bahari na pwani, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kudhibiti uchafuzi na kuendeleza miradi ya Uchumi wa Buluu.

“Lengo la Serikali ni kuhakikisha fursa za Uchumi wa Buluu zinawafikia wananchi, hususan jamii zinazotegemea bahari na pwani,” amesema Masauni.

Ameeleza kuwa fursa hizo ni pamoja na ajira, uvuvi endelevu, ufugaji viumbe maji, utalii, biashara, huduma na kuongeza thamani ya mazao.

Aidha, amesema COP12 itatoa fursa ya kuunganisha Tanzania na mifuko ya kimataifa pamoja na taasisi za fedha kwa ajili ya miradi ya uhifadhi wa bahari na pwani, mabadiliko ya tabianchi, uchafuzi na bioanuwai.

Masauni amesema mkutano huo pia utatumika kuimarisha utekelezaji wa Marine Spatial Planning (MSP), pamoja na kupata utaalamu, teknolojia na ushirikiano wa kikanda katika kupanga matumizi endelevu ya maeneo ya bahari.

Amesema Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imeanzisha Kitengo mahsusi cha kuratibu maendeleo ya Uchumi wa Buluu, unaohusisha matumizi endelevu ya rasilimali za bahari kwa ajili ya kukuza uchumi na ustawi wa jamii.

Kwa upande wa manufaa kwa jamii, amesema utekelezaji wa Mkataba wa Nairobi umechangia kuongezeka kwa uelewa wa wananchi kuhusu matumizi endelevu ya rasilimali za bahari na pwani, pamoja na kuimarika kwa shughuli za kujipatia kipato kwa jamii za wavuvi.

Amesema pia jamii zimehusishwa katika urejeshaji na uhifadhi wa misitu ya mikoko, ikiwemo Delta ya Rufiji, huku hatua za kupunguza uchafuzi wa bahari kupitia usimamizi wa taka za plastiki na maji machafu zikiendelea.

Masauni ametoa wito kwa Wizara, taasisi za umma, sekta binafsi, wanazuoni, watafiti, mashirika ya kiraia na wananchi kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika maandalizi ya COP12 ili kuongeza tija kwa Taifa.

Amesema matarajio ya Tanzania ni kuhakikisha mkutano huo unaleta matokeo yatakayolinda mazingira ya bahari na pwani, kuimarisha Uchumi wa Buluu, kuongeza ushirikiano wa kikanda na kimataifa na hatimaye kuleta manufaa kwa wananchi, hususan jamii zinazotegemea rasilimali za bahari na pwani.
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...