Na Victor Masangu, Pwani

Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Pwani, Mhe. Mariam Ibrahim, ameunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, za kuwawezesha wanawake kiuchumi kwa kuikabidhi Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT) Mkoa wa Pwani pikipiki 10 zitakazotumika kama mradi wa kuwaongezea kipato.

Mhe. Mariam amekabidhi pikipiki hizo wakati wa hafla iliyofanyika katika viwanja vya nje ya Ofisi ya Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha, ambapo amesema mradi huo utakuwa chachu ya kuwawezesha wanawake kujikwamua kiuchumi na kuondokana na utegemezi.

Amesema pikipiki hizo zitagawanywa na kutumika katika jumuiya za wanawake katika wilaya mbalimbali za Mkoa wa Pwani, kwa lengo la kuanzisha na kuendesha shughuli zitakazowaongezea kipato.

Aidha, Mhe. Mariam amesema lengo la mchango huo si kujinufaisha yeye binafsi, bali ni kusaidia jamii na jumuiya mbalimbali, huku akibainisha kuwa ameamua kutumia sehemu ya fedha za mshahara wake kutekeleza ahadi na kusaidia wanawake wa Mkoa wa Pwani.

“Nimeamua kutumia fedha zangu za mshahara kwa ajili ya kusaidia wanawake wa Mkoa wa Pwani. Nimekabidhi pikipiki 10 ambazo zitasaidia jumuiya za wanawake katika wilaya mbalimbali na mradi huu utawawezesha kujikwamua kiuchumi na kuachana na utegemezi,” amesema Mhe. Mariam.

Mbali na pikipiki hizo, Mhe. Mariam pia ametoa vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya Sh milioni 20 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa nyumba ya mtumishi wa UWT Mkoa wa Pwani.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Pwani, Zainabu Vullu, amesema jumuiya hiyo imeweka mikakati ya kuhakikisha wanawake wanaondokana na utegemezi kwa kuanzisha na kuimarisha miradi mbalimbali ya maendeleo yenye tija.

Amesema miradi hiyo inalenga kuwawezesha wanawake kuwa na vyanzo endelevu vya kipato na hivyo kuchangia maendeleo ya familia zao na jamii kwa ujumla.

Naye Katibu wa UWT Mkoa wa Pwani, Aziza Omary, amempongeza Mhe. Mariam Ibrahim, ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza Kuu la UWT Taifa, kwa msaada wa pikipiki hizo 10 pamoja na vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya Sh milioni 20.

Amesema msaada huo utasaidia kuimarisha shughuli za UWT katika ngazi ya Mkoa na wilaya, huku mradi wa pikipiki ukitarajiwa kuwa chachu ya kuwawezesha wanawake kiuchumi na kuongeza uwezo wao wa kujitegemea.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...