Mkurugenzi wa Vodacom Business wa Vodacom Tanzania PLC, Nguvu Kamando (kushoto), akikabidhi tuzo kwa mshindi wa kwanza wa mashindano ya Vodacom Coastal Classic upande wa wanawake, Mary Aleper (katikati) kutoka Uganda. Washindi wengine wa mashindano hayo walikuwa Ditona Munu Martinie mshindi wa pili kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) (wa pili kushoto) na Mercy Elegae kutoka Kenya, aliyeshika nafasi ya tatu.
Washindani wa mashindano ya Vodacom Coastal Classic wakiwa katika eneo la kuanzia mashindano hayo kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, kuelekea Bagamoyo, wakimsikiliza Mkurugenzi wa Tehama wa Vodacom Tanzania Plc Athumani Mlinga

Mshindi wa Kwanza wa Mashindano ya Vodacom Coastal Classic upande wa wanaume Charles Kagimu kutoka Uganda (katikati) mshindi wa pili Jordan Schleck kutoka Uganda (kushoto) na mshindi wa tatu Boniphace Ngwata kutoka Tanzania (kulia), wakionesha mfano wa hundi walizokabidhiwa katika mashindano hayo. Washindi hao walijishindia milioni 10 kwa mshindi wa kwanza, milioni 7 kwa mshindi wa pili, na milioni 5 kwa mshindi wa tatu mtawalia.
Washiriki wa Mashindano ya Nyerere Cycling Tour wakiendelea na Mashindano hayo ukanda wa Pwani wa bahari ya Hindi kuelekea Bagamoyo

Mkurugenzi wa Vodacom Business kutoka Vodacom Tanzania PLC Nguvu Kamando (kulia), na mwanzilishi wa msafara wa baiskeli wa Nyerere Cyling Tour Gabriel Landa kushoto, wakiwa kwenye picha ya pamoja na washindi wa mashindano wa Cycling Tour Upande wa wanawake, Mary Aleper kutoka Uganda aliyeshika nafasi ya kwanza (katikati), Ditona Munu Martinie kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) aliyeshika nafasi ya pili (wa pili kushoto), na Mercy Elegae kutoka Kenya aliyeshika nafasi ya tatu (wa pili kulia). Washindi hao walijishindia kiasi cha shilingi milioni 10, milioni saba na milioni tano kila mmoja.



               ========. ========. ========. ==========



Vodacom Coastal Classic Yaunganisha Michezo, Utalii na Maendeleo ya Vijana Africa

Bagamoyo, Pwani - 4 Oktoba 2026: Uzinduzi wa mashindano ya Vodacom Coastal Classic umeonesha namna ambavyo michezo inaweza kuwa chachu ya kukuza utalii, elimu na maendeleo ya jamii, huku mashindano hayo ya kuendesha baiskeli yakitoa fursa ya kuonesha vivutio vya utalii vilivyopo katika ukanda wa pwani ya Tanzania na kuunga mkono shughuli zenye manufaa ya muda mrefu kwa jamii ambazo msafara wa waendesha baiskeli wa Nyerere Cycling Tour (zamani Twende Butiama) utapita.

Kwa kuwakutanisha waendesha baiskeli, jamii na wadau mbalimbali, mashindano hayo yametoa mchango katika kukuza utalii wa ndani, kuhamasisha vijana kupitia michezo na kusaidia jitihada za elimu na maendeleo katika maeneo yanayounganishwa na safari hiyo.

Mashindano hayo, ambayo ni sehemu ya maandalizi kuelekea msafara wa Nyerere Cycling Tour, yaliwakutanisha waendesha baiskeli 147 walioshiriki mbio hizo zilizopita katika maeneo ya kuvutia ya ukanda wa pwani ya Tanzania. Mbali na kutoa ushindani kwa waendesha baiskeli, mashindano hayo yameendelea kuonesha fursa za utalii nchini na kuongeza uelewa kuhusu shughuli za elimu, afya na uhifadhi wa mazingira zitakazotekelezwa katika maeneo mbalimbali wakati wa safari ya msafara huo kuelekea Butiama.

Afisa Mwandamizi wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT) Charles Maguzu aliwapongeza waandaaji na washiriki wa mashindano hayo kwa kutumia michezo kama jukwaa la kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi, huku ikiendelea kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kituo cha utalii wa michezo.

“Vodacom Coastal Classic ni ushahidi wa namna mchezo wa baiskeli unavyozidi kuwa na nafasi muhimu katika kuhamasisha maisha yenye afya, kutoa fursa kwa vijana wenye vipaji na kuonesha vivutio vya utalii vya Tanzania. Kupitia matukio kama haya, hatuendelezi vipaji vya michezo pekee, bali pia tunachangia katika elimu, uelewa kuhusu uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya jamii. Tunawapongeza Vodacom na washirika wote kwa kuendelea kuwekeza katika kukuza mchezo huu na kuhamasisha kizazi kijacho cha waendesha baiskeli,” alisema.

Baada ya ushindani mkali, Charles Kagimu Kutoka Uganda na Mary Aleper kutoka Uganda waliibuka washindi wa mashindano ya Vodacom Coastal Classic 2026 baada ya kumaliza katika nafasi ya kwanza kwa upande wa wanaume na wanawake, ambapo kila mmoja alizawadiwa shilingi milioni 10.

Mashindano hayo yaliwapa waendesha baiskeli fursa ya kutumia vipaji vyao kama chanzo cha kipato kupitia ushindani wa kitaaluma, huku yakihamasisha vijana zaidi kushiriki katika mchezo huo.

Washindi wa nafasi ya kwanza katika kila kundi walipata shilingi milioni 10, huku washindi wa nafasi ya pili wakipata shilingi milioni 7 na nafasi ya tatu shilingi milioni 5. Waendesha baiskeli waliomaliza katika nafasi ya nne hadi ya kumi katika kila kundi walizawadiwa shilingi milioni 1 kila mmoja.

Akizungumza baada ya mashindano hayo, Mkurugenzi wa Vodacom Business wa Vodacom Tanzania PLC Nguvu Kamando, aliwapongeza washindi pamoja na waendesha baiskeli wote walioshiriki, akieleza kuwa mashindano ya Vodacom Coastal Classic yataendelea kutoa fursa kwa waendesha baiskeli kuonesha vipaji vyao huku yakichangia katika malengo mapana ya maendeleo ya taifa.

“Zaidi ya ushindani wenyewe, Vodacom Coastal Classic na Nyerere Cycling Tour zinasaidia kukuza utalii wa ndani, kuunga mkono shughuli za elimu na kuhamasisha matokeo chanya ya kijamii katika jamii zinazopitiwa na safari hii. Tunajivunia kuwa sehemu ya jukwaa linalowawezesha vijana, wakiwemo wasichana, huku likitumia michezo kama nyenzo ya kuchochea maendeleo,” alisema.

Kwa upande wake, Meneja wa Uendelevu wa Stanbic Bank Tanzania, Annette Nkini, alisema ushirikiano huo unaonesha dhamira ya benki hiyo katika kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi hapa nchini.

“Kwa miaka 30, Tanzania imekuwa zaidi ya soko kwa Stanbic Bank; ni nyumbani kwetu. Vodacom Coastal Classic na Nyerere Cycling Tour vinaonesha uwezo wa Tanzania katika utalii, vinawekeza katika elimu na vinafungua fursa kwa vijana na jamii kustawi. Kupitia ushirikiano huu tunawekeza kwa watu na jamii ambao maendeleo yao yataendelea kuijenga Tanzania ya kesho," alisema.

Aliongeza kuwa Stanbic Bank itaendelea kuunga mkono mashindano hayo kupitia ushirikiano wake katika Nyerere Cycling Tour na jitihada za kuhamasisha Watanzania wengi zaidi kushiriki mchezo wa baiskeli kama fursa ya michezo na uchumi.Vodacom Coastal Classic ni sehemu ya shughuli zinazoambatana na Nyerere Cycling Tour, ambayo itahusisha safari ya kilomita 1,500 kutoka Dar es Salaam hadi Butiama kuanzia tarehe 5 hadi 14 Oktoba 2026. Safari hiyo itawakutanisha waendesha baiskeli kutoka Tanzania na nchi nyingine, sambamba na shughuli zinazolenga kuhamasisha elimu, afya na uhifadhi wa mazingira katika maeneo mbalimbali yatakayopitiwa.

Kampuni ya Vodacom Tanzania ndyo mshirika mkuu wa Nyerere Cycling Tour, huku Afro Oil, Stanbic Bank Tanzania, BYD, ABC, Coca-Cola na Huawei zikiwa miongoni mwa washirika wanaounga mkono mpango huo kwa ujumla.

Kumalizika kwa mashindano ya Vodacom Coastal Classic sasa kunaweka msingi wa kuendelea kwa safari ya Nyerere Cycling Tour, huku waendesha baiskeli wakijiandaa kuendelea na safari kuelekea Butiama, nyumbani kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...