WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amewataka wakuu wa mikoa kuandaa mipango mahususi yenye malengo yanayopimika ili kuongeza kasi ya matumizi ya nishati safi ya kupikia katika taasisi na kaya nchini.
Maelekezo hayo yanakuja wakati taarifa ya Wizara ya Nishati ikionesha kuwa taasisi 2,703 kati ya 31,395 zinazolengwa nchini zimehamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Dkt. Mwigulu ametoa maelekezo hayo leo (Jumamosi, Novemba 28, 2026) wakati akihitimisha kikao kazi kuhusu utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa Mwaka 2024–2034, kilichofanyika katika Ukumbi wa Kambarage, Hazina Square, jijini Dodoma.
Amesema kila mkoa unapaswa kutambua taasisi zinazohitaji kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi na kuweka malengo ya utekelezaji, hususan katika shule za bweni, vyuo na magereza.
“Natamani kuona kila mkoa ukiandaa mpango mahususi kufuatana na eneo lake,” amesema
Ametoa mfano wa mkoa wenye shule 20 za bweni kuweka lengo la kuhamishia shule 10 kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kurahisisha ufuatiliaji wa utekelezaji.
Aidha, ameelekeza wizara na wakuu wa mikoa kupitia hatua kwa hatua maelekezo yaliyotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa uzinduzi wa mkakati huo Mei 8, 2024, ili kubaini yaliyotekelezwa na ambayo hayajakamilika.
Waziri Mkuu pia amewataka wakuu wa mikoa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu manufaa ya nishati safi ya kupikia, kushirikisha sekta binafsi na kuandaa mipango ya kupanda miti na kurejesha uoto katika maeneo yaliyoharibiwa.
Amesisitiza kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia yanahusisha afya, mazingira, uchumi na uwezeshaji wa wanawake na vijana, hivyo mafanikio ya mkakati huo yanapaswa kupimwa kwa matokeo ya utekelezaji wake.
Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Felchesmi Mramba, amesema matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini yameongezeka kutoka asilimia 6.9 hadi asilimia 28.6 mwaka 2025, huku yakikadiriwa kufikia asilimia 35 mwishoni mwa mwaka 2026.
Amesema lengo la mkakati huo ni kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034, huku majiko banifu 145,659 na mitungi 484,410 ya gesi ya kupikia ikiwa imesambazwa katika maeneo mbalimbali nchini.
.jpeg)



.jpeg)

.jpeg)




Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...